KAIMU kocha mkuu wa timu ya Taifa Stars, Hemed Morocco ametangaza kikosi cha wachezaji 23 watakaoshiriki katika maandalizi ya michezo miwili ya kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DR Congo).
Tanzania ambayo ipo kundi H ikiwa na pointi nne baada ya kutoka suluhu dhidi ya Ethiopia kisha kuwafunga Guinea, itakuwa na kibarua kizito katika michezo hiyo inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 10 na 15 dhidi DR Congo wanaoongoza msimamo wa kundi hilo na pointi sita.
Katika uchaguzi wake, kocha Morocco pamoja na jopo lake la ufundi, ameeleza kikosi kimechaguliwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia mahitaji ya kiufundi na mbinu za mchezo zinazohitajika ili kukabiliana na DR Congo, timu yenye uzoefu mkubwa kwenye mashindano ya kimataifa.
“Tumezingatia uwezo wa kila mchezaji na jinsi wanavyoweza kuchangia kwenye mbinu zetu kwa ajili ya michezo hii. Ni muhimu tukafanikisha lengo letu la kufuzu na tunaamini kikosi hiki kitafanya vizuri,” amesema Morocco.
Morocco amechagua wachezaji ambao ni mchanganyiko wa wazoefu na vijana wenye vipaji vinavyochipukia. Lengo la kuchanganya makundi haya amesema ni kuhakikisha timu ina nguvu kwenye kila safu kuanzia ulinzi, kiungo hadi safu ya ushambuliaji.
Wachezaji wazoefu akiwemo nahodha wa kikosi hicho, Mbwana Samatta aliyekosekana dhidi ya Ethiopa na Guinea wanaaminika ataleta uzoefu na utulivu kwenye timu, huku vijana chipukizi wakitarajiwa kuleta nguvu mpya na kasi itakayowasumbua wapinzani.
Katika mchezo wa kwanza, Taifa Stars itakutana na DR Congo ugenini na mchezo wa pili utafanyika nyumbani Tanzania. Michezo yote miwili ni fursa ya Taifa Stars kuonyesha uwezo wao na kuwania nafasi ya kushiriki michuano mikubwa ya soka barani Afrika. DR Congo ni timu ngumu na yenye historia nzuri katika soka la Afrika, lakini Kocha Morocco anaamini kikosi chake kina uwezo wa kuleta ushindani mkali na kufuzu kwa michuano hiyo.
KIKOSI KAMILI
Makipa; Ally Salim (Simba), Zuberi Foba (Azam FC) na Yona Amos (Pamba)
Mabeki; Mohammed Hussein (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Pascal Masindo (Azam), Ibrahim Hamad (Yanga), Dickson Job (Yanga), Bakari Mwamnyeto (Yanga), Abdulrazack Hamza (Simba) na Haji Mnoga (Salford City, England).
Viungo; Adolf Mtasingwa (Azam), Habib Khalid (Singida Black Stars), Himid Mao (Talaal El Geish, Misri), Mudathir Yahya (Yanga), Feisal Salum (Yanga), Seleman Mwalim (Fountain Gate), Kibu Denis (Simba), Nasoro Saadun (Azam) na Abdullah Said (KMC).
Fowadi; Cyprian Kachwele (Vancouver Whitecaps, Canada), Celement Mzize (Yanga), Mbwana Samatta (PAOK, Ugiriki).