Polisi wakamata shehena ya mafuta ya kula baharini

 

JESHI la Polisi, Kikosi cha Wanamaji Dar es Salaam, limekamata mafuta ya kula lita 20,400 na watuhumiwa 11, waliokuwa wanayasafirisha kwa njia za magendo kutoka bandari bubu ya Zanzibar kuelekea bandari bubu ya Kunduchi. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa ya kamanda wa kikosi hicho, Moshi Sokoro, kwa umma jana ilieleza kuwa mafuta na wahalifu hao, wamekamatwa katika operesheni yake ya kudhibiti uhalifu na wahalifu, katika Ukanda wa bahari ya Hindi.

Amesema operesheni hiyo iliyofanyika kwa siku 30 kuanzia tarehe 01 Septemba 2024, ililenga kuimarisha ulinzi na usalama wa raia pamoja na vyombo vyote vya uvuvi na usafirishaji, vinavyofanya kazi katika ukanda wa bahari.

“Manahodha nane walikamatwa kwa kosa la kukwepa ushuru wa forodha wakiwa na majahazi mawili Z.2491 MV Niazao, ikiwa imebeba madumu 370 ya lita 20 ya mafuta ya kupikia aina ya Hayat na Z. 2646 MV. Iqra, ikiwa imebeba madumu 650 ya mafuta ya kupikia aina ya Premiere ya lita 20, jumla ya madumu yalilyokamatwa ni 1020,” amesema.

Kwa mujibu kamanda Sokoro, kikosi hicho kimekamata boti moja ndogo inayoitwa MV. Zanzibar One, ikivusha abiria kwa njia hatarishi maeneo ya Ferry Magogoni; na mtuhumiwa mmoja alikamatwa na kulipa faini kwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

“Pia lipo tukio la ajali ya boti kugongana na boti nyingine na kusababisha majeruhi, tukio hili limetokea Septemba 26, 2024 eneo la Ferry Magogoni, ambapo boti ndogo mbili MV. Tawaqal iligonga MV. bozen 2 katika harakati za kuvusha abiria na kusababisha majeruhi Said Rashid (38), mkazi wa Mbagala ambaye alikuwa ni miongoni mwa abiria waliokuwa wakivuka na boti hizo, majeruhi yupo hospitali ya Taifa Muhimbili akiendelea na matibabu,” amesema.

Ameongeza: “Jeshi la Polisi linatoa onyo kwa manahodha wa boti wasio waadilifu kwa kuwataka wazingatie taratibu zote za usalama majini, pia wafanyabiashara wote wa baharini kufuata sheria na kanuni za usafirishaji mizigo baharini. Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria kwa wahalifu wote.”

Amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo, pale wanapoona viashiria vya kutokea uhalifu ili liweze kuuzuia kabla haujatokea.

About The Author

Related Posts