Mashujaa kumwaga noti kwa mastaa kuiua Yanga

WAKATI Mashujaa FC ikibakiza mechi sita kujua hatima yake Ligi Kuu Bara, uongozi wa timu hiyo umesema utaongeza dau kwa wachezaji ili kuhakikisha kuanzia mechi ijayo dhidi ya Yanga hawaachi kitu kukwepa aibu ya kushuka daraja.

Mashujaa iliyopanda Ligi Kuu msimu huu kupitia mchujo (play Off) ilipoishusha Mbeya City kwa jumla ya mabao 3-1, kwa sasa ipo katika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 23 ikibakiza dakika 540 za jasho na damu kubaki au kushuka daraja.

Maafande hao wa mjini Kigoma baada ya kuondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho na Singida Black Stars kwa penalti 4-3 katika robo fainali, itakuwa uwanjani Jumapili kuikaribisha Yanga mechi ikipigwa Uwanja wa Lake Tanganyika.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Meja Abdul Tika amesema kwa sasa hesabu zao ni kushinda michezo sita iliyobaki ili kukwepa aibu ya kushuka daraja akibainisha kuwa upo mpango wanauseti haswa kuongeza dau kwa wachezaji wao ili wapambane uwanjani.

Amesema licha ya kwamba uongozi ulikuwa na utaratibu wa kuwapa bonasi wachezaji kila mchezo, lakini kuanzia mechi dhidi ya Yanga wanaweza kupandisha dau ili kuwapa hamasa zaidi.

“Kila mechi tulikuwa tunaweka motisha japo ni siri kwa sababu ya taratibu zetu, lakini kuanzia mechi ijayo na Yanga tutaongeza kiwango ili kuwapa nguvu wachezaji kushinda mchezo huo,” amesema Meja Tika.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Salum Kimwagu amesema pamoja na mipango ya ushindi wa mechi zote, lakini wanapambana zaidi kushinda michezo minne ya nyumbani.

Amesema baada ya mechi dhidi ya Yanga hesabu zitahamia kwa KMC, Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji, huku wakisuka mipango kwa mechi za ugenini mbele ya Tabora United na Prisons.

“Tunayo kauli mbiu mpya ya ikumbatie Mashujaa tuvuke 2024/25. Tunataka kulipa kisasi dhidi ya Yanga, lakini kupambania timu ibaki salama Ligi Kuu msimu ujao,” amesema Kimwagu.
 

Related Posts