Mbunge adai  Rais mstaafu Zanzibar anaishi kwenye hali ngumu

Dodoma. Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Suleiman Haroub Suleiman amesema Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma anaishi katika hali ngumu baada ya nyumba yake kukabiliwa na mmomonyoko wa udongo.

Dk Salmin aliwahi kuwa Rais wa Zanzibar katika kipindi cha kuanzia Oktoba 25 mwaka 1990 hadi Novemba 8, mwaka 2000.

Akiuliza swali bungeni leo Ijumaa Aprili 19, 2024, Suleiman amesema kuna baadhi ya viongozi ambao waliitumikia Serikali ya Tanzania akiwamo Dk Salmin ambaye anaishi katika hali ngumu.

Amesema ugumu huo unatokana na nyumba yake kukabiliwa na mmomonyoko wa udogo kwa sababu ipo karibu na bahari.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza  na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour Juma. Picha na mtandao

“Je, Serikali iko tayari kushirikiana na viongozi wa kamati ya baraza kuu la wawakilishi Zanzibar ili kutatua changamoto hiyo,” amehoji Suleiman.

Pia amesema kuna baadhi ya maeneo yanahitaji kutunzwa lakini hadi sasa yako katika hali hatarishi, ikiwemo shule aliyosoma Karume pasipo kueleza anamzungumzia Karume yupi.

Abeid Amani Karume ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Amani Abeid Karume, ambaye ni mwanaye pia  aliongoza Zanzibar katika wadhifa huo.

Amehoji Serikali ina mpango gani wa kukarabati maeneo hayo.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais -Muungano na Mazingira, Dk Suleiman Jafo amesema sheria inagusa maeneo mahususi, lakini kwa sababu hayo ni mambo ya Muungano atayachukua na kuyafanyia kazi kupitia wenzao wa Zanzibar.

Kuhusu ukarabati wa maeneo, Dk Jafo amesema kwa sababu ofisi yake inashirikiana vizuri na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais  Zanzibar wanalichukua na kujadiliana kuona wanafanyaje kuboresha maeneo hayo.

Katika swali la msingi, Suleiman amehoji Serikali ina mpango gani wa kuwaenzi na kuwatunza waasisi wa Muungano.

Akijibu swali hilo, Dk Jafo amesema Serikali imekuwa na utaratibu wa kuwatunza, kuzitembelea na kuzifariji familia za waasisi wa Taifa kama njia mojawapo ya kutambua mchango wa waasisi wa Muungano.

Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha kila mwaka kumbukumbu za kifo cha Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, pamoja na maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafanyika.

Related Posts