Dodoma. Je, Kenya kupata Naibu Rais mwanamke? ndivyo inavyoelekea kwa kuwa jina linalotarajiwa kumrithi Naibu Rais Rigathi Gachagua iwapo ataondolewa kwenye nafasi hiyo ni Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga, Anne Waiguru.
Anne Waiguru ndiye alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa gavana katika historia ya Kenya.
Anne Waiguru mbali na kuwa gavana mwaka 2017 aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza nchini Kenya kuchaguliwa kuwa gavana na baadaye akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa baraza la magavana.
Mwaka 2019, Waiguru alinusurika kung’olewa ugavana, hata hivyo mpango huo haukuwezekana.
Mwingine ambaye anatajwa huenda akarithi kiti cha Naibu Rais ni Waziri wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki.
Kindiki mwenye umri wa miaka 52, safari yake ya kisiasa ilianza mwaka 2013 alipochaguliwa kuwa seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi.
Waziri huyo amekuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia mwaka 2004 hadi 2005. Ni mwanasheria mzoefu na Wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya.
Hoja ya kumng’oa Gachagua
Bunge la Taifa limeanza mchakato wa kumshitaki na kumng’oa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua, baada ya Spika wa Bunge hilo, Moses Wetang’ula kuzikubali hoja 11 zilizowasilishwa na mbunge wa Kibwezi West, Mwengi Mutuse.
Jumla ya wabunge 291 kati ya 349 wa Bunge la Taifa wamesaini hoja ya kumshitaki na kumng’oa madarakani Naibu Rais, Rigathi Gachagua.
Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, chini ya Ibara ya 150, inaeleza masharti ya kuondolewa kwa Naibu Rais, ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa sheria na kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu.
Hoja ya kumshtaki ni lazima iungwe mkono na angalau theluthi moja ya wabunge (117) katika Bunge ili taratibu rasmi zianze iwapo Bunge la Kitaifa na Seneti litaidhinisha kwa thuluthi mbili ya kura nyingi.
Gachagua anaweza kuondolewa ofisini iwapo wabunge 233 na maseneta 45 wataunga mkono hoja iliyowasilishwa bungeni.
Miongoni mwa tuhuma za Gachagua ni kukiuka kifungu cha 10 cha Katiba kwamba matamshi yake hadharani yamekuwa ya uchochezi na yanaweza kuibua chuki za kikabila.
Pia, anatuhumiwa kukiuka kifungu 147, 148, 174, 186, 189 vinavyozungumzia mwenendo na wajibu wake kama msaidizi mkuu wa Rais.
Gachagua, pia anatuhumiwa kupata mali kwa ufisadi na kutumia fedha za walipa kodi kwa njia isiyo halali. Mali hizo zinasemekana kusambazwa katika kaunti za Nyeri, Nairobi na Kilifi.
Ikiwa hoja hiyo itakamilika Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetangula atawasilisha azimio la kumng’oa Gachagua madarakani ndani ya siku mbili kwa Spika wa Bunge la Seneti, Amason Kingi ili achukue hatua.
Masharti ambayo Naibu Rais anaweza kuondolewa madarakani yamebainishwa katika kifungu cha 150.
Vifungu hivi vinalinda dhidi ya kufukuzwa kazi bila sababu na kuhakikisha Naibu Rais anawajibika kwa wananchi na Katiba.
Kulingana na Katiba ya Kenya, Naibu Rais anaweza kufutwa kazi iwapo atavunja sheria, kujihusisha na tabia mbaya sana au kupoteza uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao kutokana na matatizo ya kimwili au kiakili.
Utaratibu wa kumng’oa unaanzia bungeni, kwa mbunge anayetaka kumshtaki Naibu Rais kuwasilisha azimio.
Hoja yao lazima ibainishe sababu za kung’atuliwa, kama vile ukiukaji wa Katiba au tabia mbaya.
Kifungu cha 150(1)(b) cha Katiba kinatamka ni lazima kuwe na sababu za kutosha za kushitakiwa ili kumuondoa mtu madarakani.
Katika kesi ya Gachagua, huenda hoja ikaendelea hadi awamu inayofuata iwapo kutakuwa na uthibitisho mkubwa kwamba amekiuka Katiba.
Iwapo tuhuma zitathibitika na kuungwa mkono Spika wa Bunge atateua kamati maalumu kuchunguza tuhuma dhidi ya Naibu Rais.
Wabunge wanaounda kamati hii wana jukumu la kukagua nyenzo na kuamua kama madai hayo yana uhalali. Kamati maalumu hufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ikiwa Naibu Rais alikiuka Katiba au alihusika katika utovu wa nidhamu kama inavyodaiwa.
Baada ya kukamilisha majukumu yao, wabunge watawasilisha matokeo yao kwenye Bunge.
Katika awamu hii, Naibu Rais anapewa nafasi ya kujitetea na kujibu tuhuma hizo.
Ni muhimu kutambua kwamba uchunguzi huo unahakikisha haki katika mchakato wa kumshtaki kwani Naibu Rais anapewa fursa ya kujitetea.
Wabunge watapiga kura kuhusu kumng’oa Naibu Rais kufuatia kuwasilishwa kwa matokeo hayo, Bunge linapiga kura ya kukubali mapendekezo ya kamati na maendeleo ya kesi hiyo.
Angalau thuluthi mbili ya wabunge lazima wapige kura kuunga mkono kutimuliwa kwa Naibu Rais ili mchakato wa kumshtaki uendelee.
Hii ina maana kwamba ili kumshtaki Gachagua, azimio hilo lingehitaji kuungwa mkono na takriban wabunge 233.
Leo Jumanne, baada ya hoja hiyo kujadiliwa, Spika wa Bunge hilo, Moses Wetang’ula amesema Naibu Rais atapewa saa mbili Jumanne ya Oktoba 8, 2024 ili kujitetea dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
Spika huyo amesema uamuzi huo unatokana na sababu zote zilizowasilishwa juu ya hoja ya kung’oa kuungwa mkono na wabunge.
Utaratibu wa kumng’oa utapelekwa kwenye Bunge la Seneti ikiwa Bunge la Kitaifa litatoa idhini kwa thuluthi mbili ya wengi.
Bunge la Seneti litasikiliza kesi ya kuondolewa mashitaka dhidi ya Naibu Rais. Katika hatua hii, Seneti inaunda kamati maalumu ya kumjadili Naibu Rais na kutathimini ushahidi uliotolewa na Bunge la Kitaifa.
Kulingana na uamuzi wa kesi hiyo, Seneti inaweza kuamua kuunga mkono au kukataa mashtaka hayo.
Ili uondoaji mashtaka ukamilike, angalau theluthi mbili ya maseneta lazima wapige kura kuunga mkono kuondolewa kwa Naibu Rais ofisini.
Hiyo inafanya kazi kwa maseneta 45 kati ya 67.
Ikiwa Seneti itapiga kura ya kumshitaki, Naibu Rais atafukuzwa kazi mara moja, na mkuu wa nchi atateua Naibu Rais mpya.
Katika kujitetea, Gachagua amekanusha madai yote dhidi yake, likiwamo dai kwamba alimshinikiza Rais William Ruto kumpa Ksh. bilioni 8 (Sh168 bilioni) ili awe tayari kuachia nafasi yake.
Akihojiwa na kituo cha redio, Gachagua alisema, “Sina tamaa ya fedha. Ningekuwa na tamaa, ningenunuliwa na wapinzani ili nitengane na Rais Ruto. Watoto wangu ni wakubwa, mke wangu ni mchungaji, fedha sio kipaumbele changu.”
Muswada wa kumwondoa Gachagua kutoka nafasi ya Naibu Rais unatarajiwa umewasilishwa bungeni leo Jumanne, Oktoba 1, 2024, kutokana na tuhuma mbalimbali kama kuchochea chuki miongoni mwa wananchi, kueneza ukabila, na ufisadi.
Katika kujibu shutuma hizo, Gachagua amejigamba kwamba yeye ndiye aliyechangia pakubwa ushindi wa Rais William Ruto kwenye uchaguzi wa 2022, akibadili jina lake kwenye karatasi za kupiga kura, Ruto asingeshinda urais wa Kenya.
Hata hivyo, sasa anamtuhumu Rais Ruto kwa kupanga njama za kumwondoa madarakani, ikiwamo kuwahonga wabunge ili waunge mkono hoja ya kumng’oa.
“Acha kuwapa wabunge fedha ili wanifukuze kazini, sitakubali jitihada zao. Wanataka nijiuzulu, lakini sitaki,” alisema Gachagua kwa lugha yake ya asili.
Pia, alimkumbusha Rais Ruto kuheshimu wapiga kura wa Mlima Kenya, akisema anatakiwa kumruhusu amalize muhula wake kabla ya kumchagua yeyote mwingine kwa ajili ya uchaguzi wa 2027.
Gachagua anakabiliwa na tuhuma za kuvunja sheria na Katiba, matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi, ukabila, vitisho kwa watumishi wa umma na hata kugomea uamuzi wa baraza la mawaziri, pamoja na kufadhili maandamano ya “Gen Z.”
Katika mahojiano ya hivi majuzi na runinga ya Citizen, Naibu Rais Rigathi Gachagua alieleza wazi jinsi uhusiano wake na Rais William Ruto umedorora.
Gachagua alifichua hali hiyo imefikia hatua ya yeye kuondolewa kwenye kundi la WhatsApp la Rais, hatua ambayo aliichukulia kama dhihaka na udhalilishaji.
Aliendelea kusimulia jinsi alivyokaribishwa wakati wa ziara ya Mfalme Charles III nchini Kenya, akidai maofisa wa Serikali walitoa picha za kumkejeli.
Aidha, alimtaka Rais Ruto kutimiza ahadi yake kabla ya uchaguzi ya kutomruhusu yeyote ndani ya Serikali kumdhalilisha Naibu Rais, huku akiashiria kuwa uhusiano wao unazidi kuzorota.
Katika mahojiano ya mwaka wa 2022, Ruto alikuwa ameapa kulinda hadhi ya Naibu Rais, akipinga uwezekano wa tofauti yoyote kati yao. Katika mahojiano hayo kwenye runinga ya NTV, Ruto alikataa uwezekano wa kutoelewana na Gachagua iwapo wangeshinda uchaguzi wa urais, akisema:
“Nataka nikwambie Joe, haya unayoyasema hayatatokea. Sitakubali Naibu Rais kudhalilishwa na wafanyakazi wa chini.”
Alipoulizwa atachukua hatua gani endapo tofauti zitatokea, Ruto alisisitiza kuna sheria za kushughulikia suala hilo, akimaanisha kwamba iwapo Gachagua atatumia madaraka vibaya, sheria itafuata mkondo wake.
Ilivyokuwa kwa Kenyatta na Ruto
Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto walikuwa washirika wa karibu waliosaidiana katika uchaguzi wa 2013 na 2017, lakini uhusiano wao ulianza kuyumba baada ya kushinda muhula wa pili wa urais mwaka 2017.
Migogoro yao iliathiri siasa za Kenya na kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama tawala cha Jubilee.
Uhuru Kenyatta na William Ruto walikuja pamoja mwaka 2013 baada ya kushirikiana katika muungano wa Jubilee.
Wote wawili walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Baada ya uchaguzi wa 2017, uhusiano kati ya Uhuru Kenyatta na William Ruto ulianza kudorora. Baadhi ya sababu kuu za kutokuelewana ni pamoja na:
Maridhiano (Handshake) na Raila Odinga: Mnamo Machi 2018, Uhuru Kenyatta alifanya hatua ya kihistoria ya maridhiano na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, maarufu “Handshake”.
Hatua iliyokuja bila kumshirikisha Ruto na ilitafsiriwa na wafuasi wa Naibu Rais kama usaliti.
Ajenda ya Mageuzi ya Kikatiba (BBI): Uhuru na Raila walitumia maridhiano yao kuanzisha mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa Building Bridges Initiative (BBI).
Mpango huu ulionekana kama jaribio la kubadilisha mfumo wa Serikali na hata kuongeza nafasi za uongozi kama Waziri Mkuu, kitu ambacho kiliwafanya wafuasi wa Ruto kuhisi kuwa mpango huo ulikuwa na nia ya kumzuia Naibu Rais kufikia urais mwaka 2022.
Ruto alipinga vikali BBI, akidai kwamba ulikuwa mpango wa kisiasa uliolenga kupanua madaraka badala ya kushughulikia matatizo halisi ya wananchi.
Pia, Kenyatta alionekana kupunguza majukumu ya Ruto serikalini.
Alianza kumpa waziri wa mambo ya ndani, Fred Matiang’i, mamlaka ya kuratibu shughuli za Serikali, majukumu ambayo awali yalikuwa yanafanywa na Naibu Rais.
Hili lilimnyima Ruto ushawishi serikalini na kuashiria mgawanyiko kati yao. Ruto alianza kufanya mikutano ya kisiasa akidai kuwa alikuwa amepokonywa mamlaka serikalini.