Dar es Salaam. Serikali imeombwa kuendelea kushirikiana na wadau kuwawezesha watoto wenye changamoto ya ulemavu wa akili na mtindio wa ubongo ili kupata ujuzi kuwawezesha kujiajiri.
Pia, imeombwa kutoa elimu kwa jamii, wakiwamo wazazi wa watoto wenye changamoto hizo ili kuondoa unyanyapaa.
Mkugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mafiga Women & Youth Development Organization (Mwayodeo), Venance Mlali amesema hayo leo Oktoba Mosi, 2024 wakati wa kikao kazi cha kujadili mradi uliolenga kuwawezesha watoto wenye ulemavu wa akili kupata elimu ya ufundi stadi.
Mradi huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) na Serikali ya Finland.
Mlali amesema kutokana na dhana potofu zilizopo katika baadhi ya jamii, kundi hilo limekuwa likibaguliwa na wakati mwingine kunyimwa haki za msingi, ikiwamo kupatiwa elimu.
Amesema watoto wenye ulemavu wa akili wakipewa ujuzi na kupatiwa fursa wanaweza kutekeleza majukumu yao kama ilivyo kwa watu wengine.
Ametoa mfano kupitia mradi wa mafunzo ya amali kwa vijana wenye ulemavu wa akili walioufanya kwa takribani miaka minne katika halmashauri za Morogoro Mji na Ifakara wamewafikia vijana takribani 181 ambao baadhi wamejiajiri na wengine wameajiriwa katika sekta mbalimbali.
Vijana hao wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 35 wamesema wamefundishwa ujuzi katika fani za upishi, ushonaji, uashi, fundi bomba na nyinginezo katika vyuo vya ufundi katika halmashauri hizo na sasa wanajipatia kipato kupitia ujuzi huo.
“Vijana wenye ulemavu wa akili wakipewa ujuzi na kuwezeshwa wanaweza kufanya shughuli za kiuchumi kama ilivyo kwa watu wengine wasio na ulemavu,” amesema.
Dk Gervas Kawonga kutoka Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa amesema jitihada hizo zimesaidia kubadilisha fikra za baadhi ya watu katika jamii baada ya kuona wanaweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama ilivyo kwa watu wengine.
Mkurugenzi wa Elimu Maalumu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Magreth Matonya ametoa wito kwa jamii, wazazi na walezi wakiwamo kuacha kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu wa akili bali wawawezeshe kupata elimu na ujuzi waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Amesema elimu kwa jamii inapaswa kutolewa ili kuachana na dhana potofu dhidi ya kundi hilo.
“Kuna jamii mtu akipata mtoto mwenye ulemavu wanachukulia kama ni laana na mkosi katika familia, dhana hizi potofu zinatakiwa kuondolewa kwa kuendelea kutolewa elimu katika jamii,” anasema.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi kadha kuhakikisha inawaibua vijana wenye changamoto hizo na kuwasaidia kupata elimu ya amali.
Pia, wanawajengea uwezo walimu wa vyuo vya ufundi stadi nchini ili kutoa ujuzi huo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Siasa Omari, mzazi wa binti mwenye ulemavu wa akili amesema aliruhusu mtoto wake kupatiwa elimu ya amali na sasa ana furaha kwa kuwa amepata ajira na kujipatia kipato.
“Wazazi tusiwafungie watoto wetu wenye ulemavu, tuwawezeshe kwani wanaweza kuwa kama vijana wengine,” amesema.