Kaya atua Singida Black Stars

UONGOZI wa Singida Black Stars umemalizana na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omar Kaya ambaye amejiunga na timu hiyo kuongeza nguvu katika uongozi akipewa nafasi ya makamu mwenyekiti.

Kaya ambaye ana uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania ameungana na timu hiyo siku chache baada ya Agosti 30, mwaka huu kuachia ngazi Namungo kutokana na matokeo mabaya.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti kuwa kwa kutambua uzoefu wake wameamua kumchukua ili kuongeza nguvu kwa lengo la kujenga timu imara na shindani.

“Sio tetesi ni kweli Singida Black Stars tumemuhitaji  Kaya kuja kuongeza nguvu kwenye uongozi wa timu yetu katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Klabu tunaheshimu mchango wake kwenye soka la Tanzania,” kimesema chanzo hicho na kuongeza:

“Kila mtu anamfahamu Kaya ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa na mpira wa Tanzania ndio maana tukaona ni mtu sahihi wa kuwa nae kwenye safari ya mafanikio ya Singida Black Stars. Tayari amesharipoti kazini na ameanza majukumu mara moja.”

Mwanaspoti lilipomtafuta Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Masanza kwa ajili ya kuthibitisha taarifa hiyo amekiri kuwepo mazungumzo na kiongozi huyo na kuweka wazi kuwa mambo yakienda sawa watatoa taarifa.

“Kuna mazungumzo yanaendelea kwa ajili ya kumalizana na kiongozi huyo mzoefu wa soka letu nafikiri ni suala la muda tu mambo yakienda sawa taarifa itatolewa,” amesema Masanza.

Related Posts