Sh121 milioni kuwezesha bunifu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Dar es Salaam. Wajasiriamali wenye ubunifu wametengewa Sh121.19 milioni kwa ajili ya kuiwezesha kununi na kutengeneza teknolojia zitakazoiwezesha jamii kupambana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Bunifu hizo ni uundaji wa vifaa vya kuhifadhia maji na vifaa vya kuhisi matetemeko.

Mkakati huo unatokana na programu ya uwezeshaji ya ClimAccelerator ikishirikiana na Smartlab chini ya Smart African Group yenye lengo la kuchochea uvumbuzi na kuja na suluhisho la kibiashara kwa kutoa mafunzo, ushauri na rasilimali kwa kampuni na wajasiriamali wa Tanzania. 

Akizungumza jana Jumatatu Septemba 30, 2024 kwenye uzinduzi wa pili wa programu hiyo, Mkurugenzi wa Biashara Smartlab, Larry Ayo amesema programu hiyo imelenga kusaidia kampuni mbalimbali na wajasiriamali wadogo.

“Leo tumetangaza ushirika wetu na Climate-KIC ambao ni washiriki wa Irish AID kwenye programu ya uwezeshaji yenye lengo la kuonesha na kusaidia wale wanaotengeneza bunifu zinazowezesha jamii kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Baadhi ya vigezo vya kupata ufadhili huo ni pamoja na kuwa na bunifu zenye uwezo wa kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Ayo.

Baadhi ya maeneo ya mabadiliko ya tabianchi yatakayoangaliwa ni mvua, joto kali, mafuriko na maporomoko yaliyotokea hivi karibuni.

Meneja Mkuu wa Programu, Uvumbuzi wa Masoko Climate-Kic Sophie White amesema kwa zaidi ya miaka 15, taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi na wabunifu kutoka sehemu mbalimbali duniani, ikiwawezesha kujenga biashara zenye faida na kusaidia jamii kupambana na athari za mazingira.

Related Posts