Dar es Salaam. Serikali imesema imeanza kuchukua hatua kuhakikisha ugonjwa wa Marburg hauingii nchini, ikiwa ni pamoja na kuwakinga watoa huduma za afya kupitia miongozo ya matibabu.
Hatua hiyo inatokana na nchi ya Rwanda kuripoti watu 26 kuugua Marburg, huku sita wakipoteza maisha tangu kuthibitishwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo Septemba 27, 2024.
Taarifa za awali nchini humo zinaonyesha wengi walioathiriwa ni wahudumu wa afya.
Tanzania imechukua tahadhari ya ugonjwa huo na hasa katika mikoa ya Kagera, Rukwa, Mwanza na Katavi, huku jozi za vifaa kinga zaidi ya 1,000 vikisambazwa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk John Jingu amesema hayo leo Oktoba mosi, 2024 alipofuatana na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu kutembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuona utayari wa kukabiliana na majanga ya magonjwa ya mlipuko.
“Tumewapa mafunzo watoa huduma, tunawafundisha wajikinge, wahakikishe wanazingatia kanuni za kupunguza maambukizi, kwani ni rahisi kusambaza ugonjwa unapohudumia kama hujajikinga.
“Unatoa maambukizi kutoka kwa mmoja kwenda kwa mwingine, kwa kufanya hivyo unajikinga mwenyewe unayemhudumia na familia zao,” amesema Profesa Nagu.
Amesema maeneo yenye hatari zaidi ni yaliyo jirani na Rwanda, ikiwemo mikoa ya Kagera na Katavi, ambako watumishi wa afya wamepewa mafunzo na elimu ya kujikinga wanapomhudumia mgonjwa,
“Tayari tuna vifaa kinga zaidi ya pea 1,000. Kagera tuna pea 600 na Mwanza tuna pea zaidi ya 100, tunaendelea kusambaza katika mikoa mingine hatarishi, lakini bado tunaendelea kutafuta vingine na kuongea na wadau kuhakikisha vinapatikana vya kutosha kuhakikisha watumishi wanakingwa pia wanafuata miongozo,” amesema.
Dk Jingu amesema wanafanya ufuatiliaji katika mipaka ya nchi kavu, bahari, maziwa na viwanja vya ndege.
“Ugonjwa huu ni hatari na unaleta maafa. Mwaka jana tulipata matukio ya Marburg kule mkoani Kagera tukaweza kuudhibiti. Kama nchi tunachukua tahadhari kwa kuhakikisha mipaka yetu iko salama, maeneo yote ya njia za kuingia nchini kupitia viwanja vya ndege, tunaweka usimamizi mzuri tunaweza kuwabaini na kuwatambua wenye ugonjwa huo na mengine ya milipuko,” amesema.
Dk Jingu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanza kutoa taarifa kwa njia mbalimbali, ikiwemo vipeperushi katika maeneo yote.
“Tunatoa elimu endelevu ili watu wachukue tahadhari na njia ni zilezile tulizojikinga kwa Uviko-19; kunawa mikono, vitakasa mikono, kujiepusha kugusana na mtu anayeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
“Majimaji yanayotoka kwa mgonjwa inaweza kuwa mate, jasho, damu au maiti ya mtu aliyefariki kwa ugonjwa kama huo ni vitu tunavyoendelea kuvifanyia kazi.”
Profesa Nagu amesema dalili za ugonjwa huo ni homa, kupatika, kuharisha, kuumwa mwili na kutoka damu maeneo ya wazi, hivyo amewataka Watanzania waonapo dalili hizo wasimeze dawa bali wafike kituo cha afya.
“Kinga ni muhimu ukiona mgonjwa anatoka damu, anatapika anaharisha usimguse, toa taarifa kwa kutumia namba ya bure 199 atapatiwa huduma hapo alipo, pia tujiepushe kuwa karibu na wanyama waliokufa, kutokula mwanayama wafu,” amesema.
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Lebba amesema wameanza kuchukua tahadhari kwa kutoa elimu kwa wananchi na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya.
“Tayari tumeanza kutoa elimu kwa watoa huduma wa kituo cha dharura cha wagonjwa, lakini pia tunafanya screening (vipimo) kwenye vituo vyote vya kuingiza watu kwenye mkoa, tunaepusha misongamano, kugusana, kukumbatiana, kushikana mikono, na kuhimiza kunawa mikono kwa kutumia majisafi na salama,” amesema.
Mganga Mkuu Mkoa wa Katavi, Jonathan Budenu amesema kwa uzoefu waliopata katika kipindi cha Uviko-19 na magonjwa mengine ya mlipuko, kuna kamati ya kudumu inayohusika na magonjwa hayo.
“Tumesikia taarifa za ugonjwa huo nchi jirani nasi tuko pembezoni, tunaimarisha huduma katika maeneo ya mipakani ili kuzuia ugonjwa huo usiingie nchini na ikitokea umeingia ni rahisi kudhibiti,” amesema.
Marburg umewahi kuibuka nchini mwaka 2023 katika Wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata za Maruku na Kanyangereko, vijiji vya Bulinda na Butayaibega ambako watu tisa waliambukizwa kati ya watatu walipona, akiwemo daktari wa kituo cha afya Maruku aliyewahudumia wagonjwa wa mwanzo na wengine sita walipoteza maisha.