Fahamu vyama vilivyotoa marais Marekani nje ya Republican, Democrats

Marekani inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Novemba 5, mwaka huu huku kampeni za uchaguzi zikitawaliwa na vyama viwili vya Republican na Democrats, ambavyo ndivyo vimetoa marais wengi nchini humo katika kipindi cha miaka 248 tangu Marekani ilipopata uhuru mwaka 1776.

Katika kipindi hicho, Marekani imetawaliwa na marais wa aina tofauti, ambao walipatikana kupitia sanduku la kura na kuliongoza taifa hilo na kulijenga hadi kuwa taifa lenye nguvu duniani kiuchumi, kijeshi na kiteknolojia.

Tangu mwaka 1789 alipoapishwa Rais wa kwanza, Marekani imeongozwa na marais 45, lakini inatambulika kwamba kumekuwa na marais 46, kwa sababu Rais Grover Cleveland alihudumu mihula miwili isiyofuatana, hivyo anahesabiwa mara mbili, kama Rais wa 22 na 24.

Marais wanne walifariki kawaida wakiwa mamlakani, ambao ni William Henry Harrison, Zachary Taylor, Warren G. Harding, na Franklin D. Roosevelt. Rais mmoja alijiuzulu, huyu ni Richard Nixon.

Vilevile, marais wanne waliuawa wakiwa madarakani, hawa ni Abraham Lincoln, James Garfield, William McKinley na John F. Kennedy).

Rais wa kwanza wa Marekani alikuwa George Washington, aliyeapishwa mwaka 1789 baada ya kupigiwa kura na wajumbe wote katika kongamano.

William Harrison alihudumu kwa muda mfupi wa siku 31 pekee, mwaka 1841 na Franklin Roosevelt ndiye Rais aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko wote, miaka 12.

Rais wa sasa ni Joe Biden, aliyeapishwa Januari 20, 2021. Yeye ameamua kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akiwa ameongoza kwa muhula mmoja wa miaka minne, sasa mchuano mkali upo kati ya Rais wa 45, Donald Trump (Republican) na Kamala Harris (Democrats).

Katika uhai wa takribani karne mbili na nusu wa Taifa la Marekani, siasa za nchi hiyo zimetawaliwa na vyama viwili vya Democrats na Republican ambavyo ndiyo vimetoa marais wengi ambapo Republican kimekuwa na marais 19 wakati Democrats kikiwa na marais 17.

Hata hivyo, walikuwepo marais wengine ambao hawakutokana na vyama hivyo, bali walitokana na vyama vingine ambavyo kwa sasa havipo tena kwenye siasa nchini humo kutokana na ukubwa wa vyama hivyo viwili ambavyo vimekuwa vikibadilishana.

Rais pekee wa Marekani ambaye hakutokana na chama cha siasa nchini Marekani alikuwa George Washington, mwasisi wa taifa hilo na Rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyeongoza kati ya 1789 – 1797.

Baada ya kuondoka kwake madarakani, Washington hakujiunga na chama chochote cha siasa kati ya vile vilivyokuwa vimeanzishwa, bali aliendelea na shughuli zake binafsi huku akiunga mkono mipango na sera za vyama zilizomvutia.

Washington alifariki miaka miwili baada ya kuondoka madarakani ambapo inasemekana kwamba katika wosia wake, alielekeza kwamba akifariki dunia, watumwa wake, takribani 390 wapewe uhuru.

Chama cha Federalist ndiyo cha kwanza cha siasa nchini Marekani na kilimtoa Rais wa pili taifa la Marekani, John Adams ambaye aliongoza kati ya mwaka 1798 – 1801.

Chama kilianzishwa kati ya 1789 na 1790 kama muungano wa kitaifa wa mabenki na wafanyabiashara katika kuunga mkono sera za fedha za Alexander Hamilton.

Walifanya kazi katika kila jimbo ili kujenga chama kilichopangwa kilichojitolea kuunda serikali itakayozingatia masuala ya kifedha na ya kitaifa. Rais pekee wa chama hiki alikuwa John Adams.
George Washington aliunga mkono mipango ya Federalist, lakini alibaki kutofungamana na chama chochote wakati wa urais wake wote.

Chama cha Federalist kiliongoza serikali ya kitaifa hadi mwaka 1801 ilipozidiwa nguvu na chama cha upinzani cha Democratic-Republican kilichoongozwa na Rais Thomas Jefferson.

Chama cha Whig kilikuwa chama cha kisiasa katikati ya karne ya 19 nchini Marekani. Sambamba na ya chama cha Democrats, kilikuwa mojawapo ya vyama viwili vikuu kati ya mwishoni mwa miaka ya 1830 na mwanzoni mwa miaka ya 1850.

Marais wanne waliotokana na chama cha Whig ni pamoja na William Harrison (1841), John Tyler (1841 – 1845), Zachary Taylor (1849 – 1850) na Millard Fillmore (1850 – 1853).

Watu wengine mashuhuri kwenye chama hicho ni Henry Clay, Daniel Webster, Rufus Choate, William Seward, John Crittenden na John Adams.

Chama cha Whig kilikuwa kinapata uungwaji mkono kutoka kwa wafanyabiashara, wataalamu, Waprotestanti (hasa wainjilisti) na tabaka la kati la mijini. Hakikupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wakulima maskini na wafanyakazi wasio na ujuzi.

Republican (Jeffersonian)

Rais wa tatu wa Marekani, Thomas Jefferson aliingia madarakani mwaka 1801 – 1809 kupitia chama cha Republican kilichokuwa na mtazamo tofauti (Jeffersonian), tofauti na chama cha Republican cha sasa.

Alikuwa mwandishi wa Katiba ya Marekani na aliyetumia nadharia ya mwanafalsafa John Locke ya “Mkataba wa Jamii” na kupanga hoja za kupinga Marekani kuendelea kuwa kwenye mfumo wa utawala wa kifalme chini ya Uingereza.

Mbali na Jefferson mwenyewe, marais wengine walioongoza kwa sera za Jefferson ni pamoja na James Madison (1809 – 1817), James Monroe (1817 – 1825). Baada ya Monroe, John Quincy Adams aliingia madaraka na kuongoza kati ya 1825 – 1829 kupitia chama cha National Republican.

Related Posts