PRESHA imeanza kupanda kuelekea dabi ya Kariakoo itakayopigwa Oktoba 19. Kambini Yanga, Kocha Miguel Gamondi kuna jambo linamfanya akune kichwa, lakini hana namna.
Simba na Yanga zinavaana kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara Oktoba 19 ikiwa ni mechi ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa baada ya timu hizo kukutana kwenye mchezo wa nusu fainali wa Ngao ya Jamii na Simba kupoteza kwa bao 1-0, Agosti mwaka huu.
Simba ambayo kwa sasa ina mabadiliko makubwa kiuchezaji imepania kufanya kitu kwenye mchezo huo kwani tambo za watani wao zimekuwa zikiwakera mitaani.
Hata hivyo, Gamondi anajiuliza mara mbili kuhusiana kumtumia kiungo wake mahiri Khalid Aucho kwenye mchezo huu kwa kuwa kwa sasa ana kadi mbili za njano na hivyo italazimika aidha kumweka benchi kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Pamba au acheze lakini kwa tahadhari kubwa kwa kuwa akipewa kadi ya tatu aikose dabi.
Kadi mbili za Aucho ambaye amekuwa mchezaji mahiri kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga kwa misimu ya hivi karibuni, moja alipewa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na nyingine alipewa kwenye mchezo wa ligi uliopita dhidi ya KMC.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa Mwanaspoti, pamoja na umahiri wa kiungo huyo, lakini kukosekana kwake kwenye dabi huenda lisiwe pigo kubwa kwa Yanga kwa kuwa tayari ameshakosa michezo kadhaa na kikosi hicho cha kocha Miguel Gamondi kikafanikiwa kutoboa kutokana na upana wa timu hiyo kwasasa sambamba na uzoefu wa mastaa waliopo.
Kiungo huyo mkabaji anayeichezea timu ya Taifa ya Uganda alikosa michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns msimu uliopita na nafasi yake alichukua Jonas Mkude ambaye alionyesha uwezo wa juu ingawa baadhi ya wachambuzi wamedai kuwa uzito wa dabi ni tofauti na mechi zingine.
Hata hivyo, Mganda huyo msimu huu pia ameshakosa mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya CBE ya Ethiopia, mechi ambayo timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 6-0.
“Nafikiri Aucho atapumzishwa kwenye mchezo dhidi ya Pamba sidhani kama tunaweza kucheza kamari kwa mchezaji mahiri kama huyu, lakini pia Mudathir Yahaya naye mechi hii dhidi ya Pamba hachezi kwa kuwa tayari ana kadi tatu za njano kwa hiyo kaeni tayari kuwaona wachezaji wengine wakicheza,” kilisema chanzo kutoka Yanga ingawa Gamondi amekuwa akisisitiza wachezaji wote ni sawa.
Yanga inaweza kuwatumia Mkude ambaye licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara lakini anaweza kuwa mtu sahihi kuziba nafasi ya Mganda huyo, wengine ni Aziz Adambwile na Salum Abubakar ‘Sure boy’ ambao wanaweza kucheza nafasi hiyo.
Mudathir alipata kadi ya tatu kwenye mchezo dhidi ya KMC lakini mashabiki wa Yanga watashangilia kwani kiungo huyo atauwahi mchezo dhidi ya Simba.
Wekundu wa Msimbazi kwao mambo yanaonekana kuwa safi kwa kuwa wachezaji wake Edwin Balua,Shomari Kapombe na Che Malone Fondoh, kila mmoja ana kadi moja tu ya njano hivyo bado wanaweza kuwatumia wachezaji wao kwenye mchezo ujao dhidi ya Coastal Union bila hofu yoyote.