Mabao matano katika mechi sita alizocheza yamemuamsha straika wa Fountain Gate, Seleman Mwalimu akielezea siri ya mafanikio yake huku akitamba kulinda nafasi yake kikosini na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Mwalimu ambaye ndio msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu amekuwa na kiwango bora akimshawishi kocha wake, Mohamed Muya kumuamini na kumpa nafasi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalimu amesema siri ni kujituma na kufuata kile anachoelekezwa na benchi la ufundi ambalo limemuamini akitamba kuwa kiu yake kila mechi ni kutengeneza nafasi na kufunga mabao.
Amesema kuitwa timu ya Taifa ni moja ya ndoto zake za muda mrefu hivyo jukumu lake ni kupambania nafasi kuitumikia nchi kwa mafanikio.
“Tunashirikiana sana na wenzangu uwanjani, lakini nafanya mazoezi binafsi na ndio siri ya mafanikio haya, ndoto zimetimia kucheza Ligi Kuu na kuitwa timu ya Taifa”
“Sijui na siwezi kutaja idadi ya mabao msimu huu nitafunga mangapi ila malengo yangu ni kuona timu inapata ushindi na kutengeneza nafasi na kufunga kila mechi ninayopangwa,” amesema Kinda huyo.
Amesema Fountain Gate haijawa na matokeo mabaya akieleza kuwa ligi ni ngumu, lakini kwa namna wanavyoenda naona mwanga wa kufanya vizuri na kumaliza nafasi za juu kwenye msimamo.