Lina PG Tour yamsogeza Mollel karibu na Dubai

Na Mwandishi Wetu

MCHEZAJI gofu ya kulipwa Nuru Mollel ana uhakika wa kutwaa ubingwa wa michuano baada ya kushinda raundi ya nne ya michuao ya Lina PG Tour mjini Moshi, ni muujiza pekee katika raundi ya tano ya michuano hiyo ndiyo itabadili muelekeo.

Mollel kutoka klabu ya Arusha Gymkhana amejiweka katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa wa michuano hiyo yenye jumla ya raundi tano baada ya kushinda raundi ya nne iliyomalizika mjini Moshi mwishoni mwa juma.

Kupitia mashindano hayo yanampa mshindi wa jumla wa raundi ya tano tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa jijini Dubai, Falme za Kiarabu.

Tishio kubwa la Mollel ni Fadhyl Nkya wa Dar es Salaam ambaye alimaliza wa pili nyuma ya Mollel katika mchuano wa raundi ya nne ambayo matokeo yake ni kama ilivyokuwa raundi ya kwanza katika viwanja vya TPC.

Katika raundi hiyo ya kwanza Mollel na Nkya walifungana kabla ya mshindi kuamuliwa kwa mashimo ya nyongeza.

Kwa muhtasari, Mollel ameshinda nafasi ya kwanza mara tatu na nafasi ya pili mara moja wakati Nkya akiwa ameshika nafasi ya pili mara mbili na hajawahi kushika nafasi ya kwanza.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa raundi ya nne ya mashindano hayo, Mollel alisema kuwa bado ni vigumu kuwa na uhakika wa ushindi kwa sababu lolote linaweza kutokea katika raundi ya tano ambayo ni ya mwisho itakayofanyika jijini Dar es Salaam mwezi ujao.

“Upinzani bado ni mkubwa wachezaji wote wanajituma sana ila nitaendelea na mazoezi ili kuhakikisha nafanya vizuri katika raundi ya tano ambayo itafanyika Dar es Salaam,” alisema Mollel

Mollel alisema anatoa ushindi wake wa raundi ya nne kwa mdhamini wa mashindano mbalimbali ya gofu na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Gofu Nchini (TGU) na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Dioniz Malinzi, kama shukrani kwake baada ya kumsaidia yeye na wenzake kuwa wacheza gofu.

“Nautoa ushindi wangu wa raundi ya nne kwa Malinzi kwa sababu yeye ndiye aliyetupika na kuiva barabara kabla ya kuichezea timu yetu ya taifa na baadaye kuwa wachezaji wa kulipwa,” alisema Mollel

Elisante Lembris ni mcheza gofu ya kulipwa kutoka Arusha alisema naye anamshukuru Malinzi kwa kutumia muda na fedha zake kuwasaidia wazawa na kuwaendeleza wacheza gofu chipukizi ambao miaka 20 baadaye wamekuwa ndiyo vinara wa mchezo katika gofu ya kulipwa.

“Kuanzia mshindi wa kwanza hadi wa 10 na hata wale ambao hawakufanikiwa kufuzu kucheza katika mchezo miwili ya mwisho, wote wamekuzwa na Malinzi. Tunashukuru sana kumuona hapa Moshi akishuhudia jinsi vijana wake wanavyofanya kazi nzuri viwanjani,” alisema Elisante ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano hayo

Hata hivyo kwa upande wa gofu ya ridhaa bado ni vigumu kutabiri mshindi wa jumla kwa sababu bado kuna ushindani mkali kati ya Ally Isanzu na Isiaka Daudi pamoja na Enosh Wanyeche ambaye amekuwa tishio kwao baada ya kushinda raundi ya nne mjini Moshi.

Isanzu mwenye alama za ushindi 1-1-5-2 ikiwa na maana ameshinda mara mbili, kumaliza wa tano mara moja na kushika nafasi ya pili mara moja ana kabiliana na Daudi ana alama 2-2-4-2 akiwa amemaliza wa pili mara mbili, kushika nafasi ya nne mara moja na nafasi ya pili mara moja.

Related Posts