Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai atalazimika kupigiwa kura ya nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kanda ya Pwani akiwa gereza la Segerea jijini Dar es Salaam.
Endapo atashinda uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumamosi Oktoba 5, 2024 Kibaha mkoani Pwani, atakuwa kada wa pili wa Chadema kushinda akiwa gerezani baada ya Ameri Nkulu kushinda udiwani mwaka 2015 huko Sumbawanga akiwa gerezani.
Ingawa chaguzi zinatofautiana, lakini Nkulu aliyekuwa akiwania udiwani katika Kata ya Lusaka, Oktoba 23, 2015 alihukumiwa kwenda jela miezi sita ikiwa ni siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu, lakini wananchi wakaamua kumchagua.
Boni Yai yuko katika Gereza la Segerea kutokana na dhamana yake kusubiri hatima ya dhamana yake ambayo imepangwa kutolewa Jumatatu Oktoba 7, 2024 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, baada ya kusogezwa hadi tarehe hiyo.
Hata hivyo, taratibu za Chadema zinaruhusu kupigiwa kura kwa staili hiyo.
Boni Yai ambaye ni mfanyabiashara, mwanaharakati na mwanasiasa wa upinzani anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mitandao ambapo upelelezi wake bado haujakamilika.
Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Septemba 29, 2024 wilayani Bagamoyo, lakini ulisogezwa mbele na waratibu wa uchaguzi huo wakisikiliza uamuzi wa mahakama wa kumpa dhamana Boni Yai ambaye ni mgombea anayechuana na Gervas Lyenda.
Septemba 27, 2024, Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Jerry Kerenge aliliambia Mwananchi: “Ngoja tuone siku hiyo (Oktoba Mosi) kutakuwa na ishu gani kuhusu mgombea huyu. Kufanya uchaguzi halafu mgombea mmoja yupo ndani (mahabusu), inawezekana hatumtendei haki, tumeamua tujipe muda kidogo.”
“Hizi ni siasa wakati mwingine unaweza ukafanya jambo kwa faida, lakini likatengeneza ugumu, tusubiri tarehe moja,” alisema Kerenge.
Hata hivyo, Jumanne Oktoba Mosi baada ya uamuzi wa mahakama kuhusu dhamana ya Boni Yai, uongozi wa Chadema Kanda ya Pwani umeamua kuendelea na uchaguzi kama ilivyopangwa ukitarajiwa kufanyika Njuwen Hoteli Kibaha badala ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Tasuba).
“Inatulazima tuendelea na mchakato kama ilivyopangwa maana hatuwezi kujua uamuzi wa mahakama utakuaje, Boni Yai atakosa fursa ya kujinadi na kuomba kura tu, kazi ambayo itafanywa na watu wake wa kampeni,” alisema mratibu huyo.
Mmoja wa wajumbe wa kamati kuu aliyezungumza na Mwananchi akiomba hifadhi ya jina amesema: “Tunalazimika kuendelea na uchaguzi kwa sababu tukiacha kuufanya unavuruga ratiba za chaguzi. Lakini kama mgombea anakubalika anakubalika tu, wapiga kura wataamua wenyewe kwani wanawajua wagombea wao wote.”
“Kitu ambacho Boni atakikosa labda ni kuulizwa maswali tu pale lakini mambo mengine yatakuwa sawa na hii kwetu si mara ya kwanza uchaguzi kufanyika na mgombea kutokuwapo, imewahi kujitokeza huko nyuma na chaguzi ziliendelea.”
Hata hivyo, si mara kwa wagombea wa nafasi mbalimbali Chadema kuombewa kura pasipo wenyewe kuwepo ndani ya ukumbi kama ilivyotokea kwa Chacha Heche aliyeibuka kidedea katika uchaguzi wa uenyekiti wa chama hicho, mkoa wa Mara, ingawa hakuwepo kwa kuwa alikuwa nje ya nchi kwa dharura.
Siyo huyo tu bali hata mbunge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule, maarufu Profesa Jay amefanikiwa kutetea kiti chake cha uenyekiti wa wilaya hiyo, wiki iliyopita baada ya kuchaguliwa tena hata hivyo hakuwepo katika ukumbi wakati mchakato huo ukiendelea kutokana na changamoto anazozipitia za kiafya.
Meneja kampeni ‘Boni Yai’
Wakati hayo yakijiri, Meneja Kampeni wa Boni Yai, Ernest Mgawe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kibamba amesema hawana wasiwasi hata mgombea asipokuwepo watamwakilisha vema katika kiny’anganyiro hicho.
“Tuendelea na maandalizi, hatuna wasiwasi hata kama chama kikiamua kuitisha uchaguzi leo, kesho tutashiriki na kumpigia kura mgombea wetu Boni Yai aliyepo gerezani.
“Tunaendelea kunadi vipaumbele vyake tangu alivyopitishwa na chama kuwania nafasi hii, tuna uhakika ataibuka kidedea katika uchaguzi huu,” amesema Mgawe aliyewahi kuwania ubunge wa Kibamba katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Wakati Mgawe akieleza hayo Lyenda amesema: “Maandalizi ya kumaliza kampeni yanakwenda vizuri kwa sababu timu yangu ya kampeni inafanya kazi nzuri tangu mwanzo, kama ambavyo timu ya Boni Yai inavyofanya.”
“Hizi kampeni zetu zinaongozwa na timu, maana hali ya siasa ya Tanzania wagombea hamuwezi kuwa mbele bali tunatanguliza timu,” amesema.
Lyenda amesema timu yake na Boni Yai zimesambaa mtaani kusaka kura kwa wajumbe wanaowaunga mkono, akisema kitendo cha mpinzani wake kusalia mahabusu hakuathiri chochote ndani ya timu yake.
“Tunamwomba Mungu tumalize salama viongozi wapatikane ili tukijenge chama kwa ajili ya maandalizi ya chaguzi zijazo za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025,” amesema Lyenda ambaye ni Ofisa Habari wa Chadema kanda ya Pwani.
Uchaguzi huo utahusisha kumpata makamu mwenyekiti ambapo mchuano upo kati ya Sheikh Ally Mohamed ‘Kadogoo’ na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kisarawe.
Pia, wajumbe wa kanda hiyo watawachagua viongozi wa mabaraza ya wazee (Baraza la Wazee la Chadema- Bazecha), Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) pamoja na mhazini wa kanda.
Kwa miaka minne, Kanda ya Pwani yenye mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Baraka Mwago, baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye aliyekuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kurejea CCM kushindwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 19, 2019.
Katika uchaguzi huo, Sumaye mbunge wa zamani wa Hanang’ na Waziri Mkuu 1995 hadi 2005 alikuwa mgombea pekee lakini akapigiwa kura ya hapana 48 na ndio 28 huku moja ikiharibika.
Katika hatua nyingine, Aden Mayala amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi, huku Belle Ponera akiibuka makamu mwenyekiti katika uchaguzi uliofanyika Septemba 29, 2024.