Huu ndiyo ukweli wa jina Debora

KWA sasa katika Ligi Kuu Bara, moja ya majina yanayoimbwa sana ni Debora Fernandes Mavambo, huku jina hilo likiacha maswali kwa mashabiki wa soka.

Hata hivyo, mwenyewe anafichua mengi kuhusu jina hilo na maana zake. Kama ilivyozoeleka ni jina la ‘kike’ kwa hapa nchini, lakini kwao alikozaliwa Angola, Congo na Gabon anakoichezea timu ya taifa hilo, maana ni tofauti.

Pamoja na hayo, kiungo huyo fundi katika mahojiano na mwanaspoti amefunguka mengi ikiwamo anataka kuacha alama Msimbazi, akitambua ukubwa wa klabu hiyo kwenye soka la Afrika na ndiyo maana haikuwa ngumu kwake kuamua kujiunga na timu hiyo.

Pia ameongelea soka la Tanzania, dabi ya Simba na Yanga na namna amekuwa akifanya mawasiliano na wachezaji wenzake wanaoongea Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa.

Mwandishi wa makala haya alimsalimia, Como você está Débora? Alicheka na baada ya hapo mwandishi alitaka kujua maana ya jina hilo ‘Debora’ ambalo liliibua utata nchini.

“Nimefurahi kusikia vile una bidii lakini Kireno ni lugha nyepesi,” anasema.

Akizungumzia kuhusu jina hilo, anasema; “Ni jina lenye maana na uzito mkubwa wa kihistoria na kitamaduni, hasa katika tamaduni za Kiyahudi na Kikristo. Debora, alikuwa nabii na hakimu katika Biblia, jina hilo limebeba ishara ya uongozi, hekima na ujasiri.”

“Katika Biblia Debora ana nafasi katika ushindi dhidi ya Wakanaani na wimbo wake maarufu wa ‘Wimbo wa Debora’, inaonyesha nguvu zake si tu katika vita bali pia katika sanaa hapo alifafanua mchezaji huyo wa Simba.”

“Maana ya jina hili pia ni ‘Nyuki’, linachochea bidii na ushirikiano kama ilivyo kwa wadudu hao wakati wakitengeneza asali, wanasifa ambazo zinaheshimiwa.”

Anasema safari yake kutoka kwenye ligi za Angola na Congo hadi Simba haikuwa rahisi kufanya mabadiliko ya ligi, lakini aliona ni fursa kwake.

“Niliona ni lazima nichukue changamoto hii kwa mikono miwili. Simba ni klabu kubwa na kuwa sehemu yake ni heshima kubwa kwangu. Nilitaka kuthibitisha uwezo wangu uwanjani na kusaidia timu kufikia mafanikio,” anasema Débora na kuongeza soka ni muhimu katika maisha yake na alianza kucheza akiwa na umri mdogo akiwa Angola na Congo na alijitahidi kila siku kuwa bora na kuaminika.

“Namna nzuri ya kukumbukwa ni kuisaidia timu kwa uwezo wangu wote kushinda makombe na kuandika historia mpya. Kila nitakapopata nafasi nitakuwa nikijitahidi kufanya vyema uwanjani na nataka mashabiki wajivunie kuwa na mimi kwenye timu hii.”

“Najua soka ni zaidi ya mchezo; ni fursa ya kuonyesha uwezo wangu na kuleta furaha kwa mashabiki. Natamani kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya klabu hii na nitajitolea kwa kila kitu kuhakikisha tunashinda kila mechi na kutimiza malengo yetu.”

Tangu ajiunge na Simba SC, Debora amekuwa kiungo wa kati mwenye nguvu, akitoa mchango mkubwa katika safu ya ulinzi na ushambuliaji. Anajulikana kwa uwezo wake wa kupiga pasi sahihi, kusoma mchezo vizuri na kuratibu mashambulizi. Katika kila mechi, ameonyesha ubora wake wa kuanzisha mashambulizi huku akihakikisha ulinzi unadumishwa imara.

“Simba ni timu ya familia. Wachezaji wenzangu wamekuwa wakiunga mkono safari yangu na hii imenipa nguvu zaidi. Tunajenga kitu cha pekee hapa na ninaamini tutafika mbali katika mashindano yote tunayoshiriki,” anasema Débora kwa kujiamini.

Kwa upande wa kiufundi, ana uwezo mkubwa wa kudhibiti kasi ya mchezo, kuhakikisha timu yake inapata utulivu inapokuwa na mpira, uwezo wake wa kuziba nafasi na kufanya kazi ya ulinzi wakati timu inaposhambuliwa. Sifa hizi zimemfanya kuwa mchezaji muhimu Simba na benchi la ufundi limekuwa likimtegemea katika michezo muhimu.

Nyota huyo ambaye ana mkataba wa miaka mitatu Simba, anajiona bado ana nafasi ya kuonyesha zaidi makucha yake kwa sababu anaendelea taratibu kuzoeana na wachezaji wenzake;

“Ndani ya muda mfupi ninajisikia furaha kuwa hapa, nilikuwa na wakati mzuri Misri ambako tuliweka kambi na kilikuwa kipindi kizuri kwangu kuanza kufahamiana na wachezaji wenzangu,”

“Nashukuru kocha alikuwa wazi kwangu na wachezaji wengine juu ya namna ambavyo nataka kuona timu ikicheza, tumekuwa tukifanya kazi pamoja ili kutoa kilichobora, binafsi najiona bado natakiwa kufanya zaidi ya hiki ambacho kwa sasa nakitoa, natakiwa kuonyesha thamani yangu zaidi.”

Debora anatambua ukubwa wa Simba na presha ambayo wachezaji wamekuwa wakikumbana nayo;  “Timu yetu ina wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa hivyo kila mmoja amekuwa akipambana kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza mara kwa mara, hilo nalo limekuwa likinisukuma pale ninapopangwa kwa kuthibitisha nastahili,” anasema Debora ambaye ana ndoto ya kucheza soka Ulaya.

Katika michezo mitano ambayo Debora amecheza ya kimashindano, mitatu ya Ligi Kuu Bara na mingine ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameonyesha ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi za kiungo wa kati na kiungo wa ulinzi.

Urefu wake wa mita 1.78 unampa faida ya kimwili uwanjani, akicheza kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu. Ameonekana kuleta utofauti kwenye eneo hilo huku akitumika sambamba na viungo wote kwa vipindi tofauti.

“Lugha ilikuwa changamoto, lakini soka lina lugha moja ambayo kila mtu anaielewa. Hii iliniwezesha kuendana na wachezaji wenzangu na kufanya kazi ya pamoja vizuri.”

Mbali na lugha, alikumbana pia na changamoto za kimbinu zinazohitaji umakini mkubwa katika ligi za Tanzania.

“Ligi ya Tanzania ni ngumu na yenye ushindani, lakini ninapenda changamoto hizi. Inanisaidia kuwa bora zaidi na kukomaa kama mchezaji.”

“Dabi ya Simba na Yanga ni zaidi ya mechi ya soka; ni utamaduni unaowaleta pamoja mashabiki wa Tanzania na hata nje ya mipaka ya nchi. Kwa muda mrefu, mechi hii imekuwa na hisia kali na nililiona hilo katika mchezo wa Ngao ya Jamii na licha ya kucheza vizuri tulipoteza dhidi ya Yanga.”

“Ni mechi inayobeba uzito wa historia, heshima na ushindani wa kweli. Kwa wachezaji, ilikuwa nafasi ya kuonyesha uwezo wetu mbele ya maelfu ya mashabiki. Naamini mchezo ujao wa dabi utakuwa tofauti kwa sababu kikosi chetu kwa sasa tunazidi kuzoeana wengi tulikuwa wachezaji wapya.”

Related Posts