Mfanyabiashara wa madini auawa mlima wa maombi, wauaji watuma meseji…

Arusha. Mwili wa mfanyabiashara wa madini ya ujenzi, David Mollel mkazi wa Kata ya Moivaro, umekutwa ukining’inia kwenye mti juu ya Mlima Oldonyowas, jirani na eneo linalotumika kwa maombi.

Inadaiwa Mollel mwenye umri wa kati ya miaka 50 na 55, aliuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Jumanne, Oktoba Mosi, 2024 kwa kunyongwa na mkanda wa suruali. Mwili wake ulifunikwa kitambaa chekundu usoni.

Taarifa za awali zinaashiria mgogoro wa kugombea eneo la uchimbaji madini ya ujenzi aina ya moramu ni chanzo cha mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha tukio hilo akisema uchunguzi umeanza kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.

Masejo amesema bado chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na wameanza uchunguzi kujua kiini cha tukio hilo kwa kushirikiana na taasisi zingine za usalama mkoani Arusha. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru.

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja na ujumbe wa vitisho uliotumwa kwa familia yake.

“Uchunguzi zaidi unafanyika kwa kushirikisha taasisi nyingine za kiuchunguzi kutokana na ujumbe wenye utata uliotumwa kwa ndugu zake watatu Septemba 30, 2024 kabla ya kugundulika kwa mwili wake katika Mlima Oldonyowas,” amesema leo Oktoba 2, 2024 alipozungumza na Mwananchi.

Wakati huohuo, jirani na rafiki wa karibu wa mke wa marehemu, Rehema John, amesema Mollel alionekana mara ya mwisho asubuhi ya Septemba 30, 2024.

Amesema alimuona saa tatu asubuhi alipokwenda kunywa chai nyumbani kwake na baadaye aliondoka.

“Jioni saa 12, rafiki yangu aliniambia anakwenda polisi kutoa taarifa maana anasikia mume wake ametekwa na watu wasiofahamika, hivyo tukaenda kutoa taarifa na kutakiwa kukaa saa 24 ndipo turudi tena,” amesema.

“Baadaye saa mbili usiku shemeji yake akampigia simu kumwambia kuna watu wametuma ujumbe kuwa wanaenda kumuua mume wake kwa sababu amekataa kuachia Mlima wa Moramu,” amesema.

Amesema familia ilianza msako na asubuhi uligundulika mwili wake katika msitu wa Mlima Oldonyowas.

Mjomba wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Mollel amesema alitumiwa ujumbe kabla ya kupigiwa simu na watu hao saa mbili kasoro usiku na kuambiwa wamepewa kazi ya kumuua ndugu yao na watu wanaogombea nao mlima na ndiyo wanaenda kutekeleza.

Ujumbe huo ambao Mwananchi umeuona unasomeka: “Unarijua hiri rijamaa renye simu hii, tunaritundika kwenye mti kakataa kuachia mgodi sio madai tu, pesa kitu gani na hiro rimoram aache, tumepewa kazi ya kumuua na watu watatu wababe akiwemo…”

“Mimi ni mmoja wa watu watatu niliotumiwa ujumbe usiku saa mbili, nikasoma nikashtuka sana maana hatujawahi kusikia ndugu yetu akiwa na ugomvi na mtu, hivyo nilimtumia kaka yangu naye asome,” amesema.

“Wakati huo nikaamua kupiga hiyo namba iliyotuma ujumbe akapokea akasema wako watatu na wamepewa pesa nyingi za kuhakikisha wanamuua ndugu yetu hivyo wanakwenda kumtundika juu ya mti,” amesema Mollel.

Steven Joram, jirani mwingine wa Mollel amesema mauaji hayo yana viashiria vya mgogoro wa eneo la uchimbaji moramu ambalo alikuwa akilimiliki.

“Alikuwa mtu wa watu sana, sijui hata huo mgodi wahusika wakiupata wataufanyia nini wakati wamedhulumu maisha ya mtu huyu aliyeacha watoto,” amesema.

Related Posts