TRA yavunja rekodi ikikusanya trilioni 3.1/= Septemba

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya Sh. 3.1 trilioni mwezi Septemba, ikivunja rekodi yake ya makusanyo kwa mara ya kwanza kufikia kiasi hicho cha fedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, aliwaambia waandishi wa habari jana Oktoba Mosi, jijini Dar es Salaam, alipokuwa anatoa taarifa ya utekelezaji na usimamizi wa mapato ya kipindi cha robo mwaka (Julai hadi Septemba), mwaka huu.

Alisema hiyo ni rekodi mpya kwa TRA kwa kuwa mamlaka hiyo haijawahi kukusanya kiwango hicho tangu kuanzishwa kwake, Julai mwaka 1996.

Alisema tangu ateuliwe kuiongoza TRA Julai mwaka huu, waliweka lengo la kukusanya Sh. 7.4 trilioni kwa robo mwaka ya kwanza (Julai hadi Septemba), na kwamba wamevuka lengo kwa kupata zaidi ya Sh. 7.7 trilioni.

Mwenda alisema mafanikio hayo yanatokana na usimamizi mzuri wa sheria za kodi, kuzuia mianya ya rushwa, kuweka mazingira rafiki ya ulipaji kodi pamoja na kusikiliza na kutatua vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara.

“Tumeandika historia mpya tangu mamlaka yetu ianze kazi. Kwa mara ya kwanza mwezi Septemba mwaka huu pekee tumefanikiwa kukusanya kodi kiasi cha zaidi ya Sh. trilioni 3.1. Ni jambo la kujivunia na kupongeza wafanyakazi na walipakodi wote nchini, mafanikio haya yanatokana na kusikiliza na kutatua vikwazo vya wafanyabiashara kwa wakati,” alisema Mwenda.

Alisema mafanikio hayo yametokana na kutimiza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeielekeza mamlaka hiyo kutimiza majukumu yake kwa uadilifu, usawa, kusimamia sera nzuri za uwekezaji na kujenga uhusiano mzuri na walipakodi.

Mwenda alisema TRA wataendelea kusikiliza wafanyabiashara, kuwafuata walipo na kuweka mazingira sawa ya kufanya biashara kila mmoja kulipa kodi stahiki bila upendeleo.

Alihimiza umuhimu wa Watanzania kudai risiti pale wanaponunua huduma au bidhaa, na wafanyabiashara kutoa risiti wakati wa ununuzi na uuzaji.

Aliongeza kuwa TRA wamekusudia kuweka nguvu na kuimarisha kitengo cha ukaguzi na uchunguzi ili kudhibiti mianya ya upotevu mapato, yakiwamo maeneo ya forodha.

Kamishna wa Forodha, Juma Hassan, alisema wanaboresha usimamizi wa mifumo ya kuhudumia wateja wao, ambayo itaanza kutumika kuanzia Januari mwaka 2025.

Kamishna wa Idara ya Walipakodi Wakubwa, Michael Muhoja, alisema asilimia 43 ya mapato ya TRA yanatokana na kodi za wafanyabiashara wakubwa.

Kamishna wa Kodi za Ndani, Alfred Mregi, aliwataka wafanyabiashara kutunza kumbukumbu zao, kutii sheria za ulipaji kodi na kuzingatia nyakati za kulipa kodi ili kuepuka faini.

About The Author

Related Posts