NUSU fainali ya kwanza ya Ngao ya Jamii kwa wanawake imetamatika mchana huu JKT Queens ikitangulia fainali baada ya kuichakaza Ceasiaa Queens kwa mabao 7-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge Dar es Salaam.
Timu zilizomaliza katika nafasi nne za juu, Simba ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu, JKT iliyomaliza nafasi ya pili, Yanga Princess (ya tatu) na Ceasiaa ndizo zinashiriki mashindano hayo ambayo yanafanyika kwa mara ya pili kupitia mfumo huu mpya.
Msimu uliopita na Simba Queens ilitwaa ubingwa wa mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa kuitoa JKT kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.
JKT ilianza kupata bao dakika ya 20 ya mchezo likifungwa na Winifrida Gerald, kisha Yasinta Mitoga akatupia la pili katika dakika ya 44, Anastazia Katunzi akaweka jingine dk45 na hat-trick ya Stumai Abdallah aliyefunga katika dakika za 45, 46 na 65 kabla ya Janet Matulanga kupigilia msumari wa mwisho katika dakika ya 87 na kuzima ndoto za Ceasiaa Queens kusonga hatua ya fainali.
Ni mara ya pili kwa JKT kama isemavyo kauli mbiu yao ya Kichapo cha Kizalendo kugawa dozi ya mabao mengi kwani msimu uliopita ilishinda 5-0 dhidi ya Fountain Gate Princess ambayo msimu huu imemaliza katika nafasi ya tano.
Matokeo hayo yanawafanya Wanajeshi hao wa kike kutangulia fainali ambayo inatarajiwa kuchezwa Oktoba 05 uwanjani hapo.