Arusha. Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumwingilia kinyume cha maumbile ndugu yao mwenye miaka 27 anayedaiwa kuwa na matatizo ya afya ya akili.
Akizungumzia tukio hilo leo Oktoba 2, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema wanawashikilia watuhumiwa hao wenye umri kati ya miaka 35 na 55 kwa mahojiano juu ya tukio hilo.
“Tukio hilo tumelipata na jalada limefunguliwa, uchunguzi umeanza dhidi ya watu watatu ambao wanahojiwa na polisi lakini hatuwezi kuwataja kwa sasa,” amesema.
Kamanda Masejo amesema upelelezi ukikamilika wahusika watafikishwa mahakamani na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.
Mwathiriwa wa tukio hilo akizungumza na Mwananchi jana Oktoba Mosi, 2024 nyumbani kwao Mtaa wa Engosemgiu, kata ya Sinon jijini Arusha, amedai ndugu zake sita wametekeleza vitendo hivyo kwa nyakati tofauti Septemba, 2024 baada ya kumlewesha kwa pombe kali.
Amedai mwanzoni mwa Septemba alipotoka kwenye msiba wa jirani, alikutana na mjomba wake mkubwa aliyemtaka amsindikize mahali.
Amedai mjomba wake alikwenda kunywa pombe na akamlazimisha naye anywe kisha akamfanyia kitendo hicho.
Amedai siku mbili baadaye mtoto wa mjomba wake alimwita akamtuma kwenda kwenye korongo lililoko mita chache karibu na nyumba yao, baadaye akamfuata na kumwingilia kwa nguvu.
“Siku hiyo jioni niko zangu nyumbani, mjomba mdogo akaniita akanituma hebu neda pale kaniangalizie kuna nini kinapiga kelele wakati nashuka akanifuata na yeye akanifanyia na kunitisha vivyo hivyo nisiseme,” amedai.
Anadai wajomba zake watano wamemfanya vivyo hivyo kwa nyakati tofauti wakiwa wanamnywesha pombe, na kwamba amechoshwa na vitendo hivyo ameamua kusema kwa mama yake mdogo.
“Hapa kwetu kuna kilabu cha pombe karibu, hivyo wakawa wananiita na kuninywesha pombe kali na kunifanyia vitendo hivyo kwa nyakati tofauti, nikachoka zaidi na kuona bora niseme waniue kuliko kuwa mtumwa, nikamwambia mama mdogo wangu,” amedai.
Jirani wa familia hiyo (jina linahifadhiwa) amesema kijana huyo amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo mara kwa mara kabla ya kuamua kusema.
“Unajua huyu kijana ni kama yatima maana baba yake alishafariki na mama ameugua ugonjwa wa akili na hayuko hapa, hivyo analelewa tu na ndugu, nadhani ndiyo wakatumia mwanya huo kumfanyia huu ukatili,” amedai.
Amedai walizaliwa watoto sita kwa baba na mama yake, yeye akiwa wa pili, dada yake ameolewa jijini Dar es Salaam na wadogo zake wawili anaishi nao hapo na wengine wako kijijini.
Jirani huyo amedai kijana huyo mwenye matatizo kidogo ya akili, ambaye muda mwingine huzubaa au kukaa sehemu moja muda mrefu, alionekana akifuatana na wajomba zake kwenye vilabu vya pombe ndipo walipoanza kutilia shaka na alipobanwa alieleza hayo.
“Baada ya kumpeleleza akasema na kutaja watu sita ambao wanne ni ndugu zake kabisa na mmoja ni kijana mkubwa wa mjomba wake na rafiki wa mjomba wake ambao ni watu wazima tena wenye wake zao hapo jirani,” amedai.
Amedai alipokiri walimpeleka hospitali ilipogundulika kuwa ameingiliwa kinyume cha maumbile hivyo walitoa taarifa polisi na watu watatu wamekamatwa, huku wengine watatu wakikimbia makazi yao.