Kwa nini ZRA imevuka lengo la makusanyo

Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imevuka lengo la ukusanyaji mapato kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25, kuimarika na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara vikitajwa kuwa miongoni mwa sababu.

Ongezeko hilo pia limeelezwa kuchangiwa na kuimarishwa mifumo na uhusiano mzuri na walipakodi, ikiwamo kusaidia kurahisisha biashara zao na kuwafikia kusikiliza changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 2, 2024 ofisini kwake, Kaimu Kamishana wa ZRA, Said Ali Mohamed amesema katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25, ilikadiriwa kukusanya Sh194.031 bilioni na zimekusanywa Sh200.934 bilioni ambao ni ufanisi wa asilimia 103.56 wa makusanyo ya mapato yaliyotarajiwa.

“Kwa kulinganisha na makusanyo halisi ya robo ya kwanza ya mwaka uliopita wa 2023/2024, yalikuwa Sh161.831 bilioni, ambayo yakilinganishwa na makusanyo halisi ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha wa 2024/25, yanaonyesha ukuaji wa makusanyo halisi wa asilimia 24.16,” amesema.

Said amesema kwa Septemba 2024, ZRA imezidi lengo kwani ilikadiriwa kukusanya Sh74.049 bilioni na imekusanya Sh76.497 bilioni, ambao ni ufanisi wa asilimia 103.31 wa makusanyo ya mapato yaliyotarajiwa.

Makusanyo halisi ya Septemba ya mwaka uliopita wa 2023/24, yalikuwa Sh61.694 bilioni, ambayo yakilinganishwa na makusanyo halisi ya Septemba mwaka huu wa fedha wa 2024/225, yanaonyesha ukuaji wa makusanyo halisi wa asilimia 23.99.

Said amesema kuimarika kwa matumizi sahihi ya mifumo katika usimamizi wa kodi, ikiwemo matumizi ya mfumo wa risiti za kielektroniki, mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa Zidras sambamba na kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya kodi kupitia njia mbalimbali kumechangia ufanisi.

Amesema mbinu nyingine inayosaidia kufikia makusanyo ni kuzungumza na wadau wa kodi kwa makundi ambayo wamekuwa wakikutana nayo kisha kuzipatia ufumbuzi kero zinazoibuliwa.

Utekelezaji wa marekebisho ya Sheria za Kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025, amesema ni hatua iliyosababisha kuimarika kwa ukusanyaji katika vyanzo vya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ushuru wa bidhaa, ada za bandari na kodi ya miundombinu.

Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha wa 2024/25 (Oktoba hadi Desemba 2024), ZRA itaendelea kufanya ziara kukutana na walipakodi kusikiliza na kutatua changamoto zao.

“Kushirikiana na jumuiya za wafanyabiashara katika kusimamia walipakodi, kuunganisha mifumo yao ya kibiashara na mfumo wa kutolea risiti za kielektroniki (VFMS) ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za walipakodi,” amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Waongoza Watalii Zanzibar (Zato), Hassan Burhan amesema hatua ya kukutana na ZRA kusikiliza kero zao imesaidia watu kuhamasika katika ulipaji kodi.

“Mfumo huu umesaidia na utasaidia kwa sababu kuna kero nyingi ambazo zinashughulikiwa kwa hiyo watu wanakuwa wepesi kulipa kodi kwani wanaona mazingira yamekuwa rafiki,” amesema.

Related Posts