Muda mfupi kabla ya Iran kurusha mamia ya makombora Israel usiku wa kumkia leo Oktoba 2, 2024, tayari bei ya mafuta imeshaanza kupanda.
Mashambulio hayo yanakuja kufuatia vita vinavyoendelea kati ya Israel na Kundi la Hezbollah la Lebanon.
Israel ilianzisha mashambulizi katika Mji wa Beirut nchini Lebanon wiki iliyopita na kusababisha mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa kundi hilo, Hassan Nasrallah.
Jana Jumanne, Oktoba 1, 2024 Ikulu ya Marekani ilitangaza inaamini Iran inajiandaa kwa shambulizi la kombora la masafa marefu dhidi ya Israel na ghafla bei ya pipa la mafuta ghafi imepanda kwa kasi kwenye masoko ya kimataifa baada ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), bei ya mafuta ya Marekani imepanda kwa asilimia 3 na kufikia zaidi ya Dola 70 za Marekani(Sh190,750) kwa pipa, huku mafuta ghafi aina ya Brent yakiuzwa kwa Dola 73 za Marekanio (Sh 198,925) kwa pipa.
Mwaka uliopita, masoko ya nishati yalionesha utulivu licha ya mvutano unaoongezeka Mashariki ya Kati, baada ya Houthi ambalo ni kundi la kiislamu na kisiasa lililoanzia Yemen miaka 1990, kuweka marufuku dhidi ya meli za mizigo kwenye Bahari Nyekundu.
Hofu kuu imekuwa juu ya kuzorota kwa hali inayoweza kusababisha Tehran kufunga mlango wa Hormuz, njia muhimu ya kusafirisha mafuta ghafi kutoka Ghuba.
Hofu hii sasa inaathiri masoko, wakati ambao benki za dunia zilikuwa zikitangaza kuwa mshtuko wa mfumuko wa bei wa miaka mitatu iliyopita ulikuwa umepungua.
BBC inaeleza kuwepo kwa hali ya wasiwasi kwamba sasa Ulaya inategemea sio tu mafuta bali pia LNG (gesi ya kimiminika inayosafirishwa ikiwa imegandishwa) kutoka Qatar, ambayo pia hupita kwenye mlango wa Hormuz, ambao ni mwembamba hadi maili 20.
Hayo yanakuja wakati tayari vita vya Russia na Ukraine vikisababisha nchi za Ulaya kutegemea soko la kimataifa la LNG.
Inaelezwa kuwa, licha ya bei za mafuta kuwa bado chini ikilinganishwa na mapema mwaka huu, mzozo wa kijiografia wa wakati mmoja unafufua kumbukumbu za enzi za mfumuko wa bei za miaka ya 1970.
Akizungumzia hali hiyo, mtaalamu wa uhusiano wa kimataifa na uchumi, Dk Wetengere Kitojo amesema athari hizo zitafika kwa nchi za Afrika.
“Unajua mara nyingi uchumi wetu unategemea sana nchi za Kiarabu kwa maana ndio chanzo kikubwa cha mafuta, kwa hiyo nchi za Kiarabu zinapoingia kwenye vita kama hivyo, kama chanzo chao kikubwa cha mapato ni mafuta, kwa vyovyote vile watataka kuongeza bei ya mafuta ili wawe na uwezo wa kugharamia,” amesema Dk Kitojo alipozungumza na Mwananchi.
“Matokeo yake sisi tutaumia, mafuta ndio chanzo cha nishati katika maeneo mengi, kwa hiyo itagusa nyanja nyingi hivyo itafanya hali ya maisha kuwa ngumu.
“Watu wanasema ukiona mwenzio wanagombana usishangilie kwa sababu naye anakuingiza vitani kwa maana maisha yanakuwa magumu,”amesema Dk Kitojo.
Mashambulio ya Iran yameongeza joto la vita kwa nchi za kiarabu, nchi angalau tisa zimejitosa kwenye vuguvugu hilo la kuishambulia Israel, zikiwamo Iraq, Syria na Yemen, huku Marekani na Uingereza zikiisaidia Israel.
Mashambulio hayo yanahusisha ndege zisizo na rubani, makombora ya cruise na makombora ya masafa marefu.
Iran ilirusha zaidi ya ndege zisizo na rubani 300 na makombora kuelekea Israel.
Shambulizi hilo lilijumuisha ndege zisizo na rubani 170 na makombora ya cruise 30, ambayo hakuna hata moja lililoingia Israel na makombora ya masafa marefu 110, ambayo machache yalifika Israeli.
Mlipuko ulianzishwa kutoka nchi kadhaa. Jeshi la Mapinduzi la Iran (IRGC) lilisema liliwarushia ndege zisizo na rubani na makombora hayo. Vyanzo vya usalama vya Iraq vilisema makombora yalionekana yakipita juu ya Iraq kuelekea Israel.
Wakati nchi hizo za Kiarabu zikiishambulia Israel, Jeshi la Marekani nalo limesema vikosi vyake vilidungua makombora na ndege zisizo na rubani kadhaa zilizorushwa kutoka Iran, Iraq, Syria na Yemen.
Jinsi ulinzi wa anga la Israel ulivyokabiliana na mashambulizi hayo ni kwamba, takriban asilimia 99 ya makombora yaliyovurumishwa yalidunguliwa nje ya anga la Israel au juu ya anga ya nchi hiyo.
Hii ilijumuisha ndege zote zisizo na rubani na makombora ya cruise. Mfumo wa Arrow ulitumika kuzuia makombora ya masafa marefu, huku Iron Dome ikiingilia kati makombora yasiyolengwa na drones.
Washirika wa Israel walisaidia pia, huku Marekani ikitumwa ndege za kivita na meli za kivita kusaidia Israel kudungua makombora na drones karibu yote yaliyovurumishwa kutoka Iran.
Rais wa Marekani, Joe Biden, alisema vikosi vya Marekani vilisaidia kudungua makombora na ndege zisizo na rubani kadhaa.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amewataka Waisraeli kufuata maagizo ya usalama na kusimama pamoja dhidi ya kile alichokiita, “mhimili wa uovu” wa Iran, akisisitiza kwamba nchi itapambana na kushinda vitisho.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917