MOROCCO kwa sasa inakamilisha maandalizi ya fainali za 35 za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika kuanzia Jumamosi ya Januari 5-26, mwakani.
Hii ni mara ya pili kwa Morocco kuandaa mashindano haya makubwa kabisa ya kandanda katika Bara la Afrika.
Mara ya kwanza ilikuwa 1988 na kukwamia katika nusu fainali baada ya kufungwa 1-0 na Cameroon iliyokuja kunyakua kombe kwa kuifunga Nigeria 1-0 katika fainali.
Morocco ambayo imeiwakilisha Afrika mara sita katika fainali za Kombe la Dunia itacheza fainali za AFCON kwa mara ya 20.
Mara nyingi ilipewa nafasi ya kubeba kombe, lakini ilimaliza safari katika robo au nusu fainali na mara moja katika fainali mwaka 2004 kwa kufungwa na Tunisia 2-1.
Sasa Morocco imepania kuhakikisha kombe linabakia kwao na kati ya hatua ilizochukua ni kuwashirikisha wachezaji mahiri wa zamani katika maandalizi.
Katika miaka ya 1960 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, Morocco ilisifika kama taifa lililoongoza kwa kandanda katika Bara la Afrika.
Hadi mwanzoni mwa karne hii ilikuwa ndoto kutarajia Morocco kufungwa na nchi ya kusini mwa Sahara, kama ilivyochapwa 3-1 na Tanzania katika kinyang’anyiro cha kugombea tiketi ya kucheza fainali za 2014 za Kombe la Dunia nchini Brazil.
Miongoni mwa wachezaji wake wengi waliong’ara sana zamani ni mchezaji wa kwanza kutoka Afrika, Larbi Ben Barek (aliyejulikana kama Almasi Nyeusi) kucheza katika ligi za Ulaya.
Sasa zaidi ya miaka 60 imepita tangu Ben Barek alipoweka historia hiyo na raia mwengine wa Morocco, Adderrahmane Belmahjoub alikuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kucheza fainali za Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa katika fainali za 1954 zilizofanyika Uswisi.
Orodha ya wachezaji mashuhuri wa Morocco wa zamani ni ndefu na miongoni mwa waliong’ara sana ni Badou Zaki, Noureddine Naybet, Tarek Dhiab, Hammad Agrebi, (Mchawi), Nejib Gommidh, Ahmed, Badou Kaki na Abdelmajid Dolmy.
Mchezaji aliyetoa mchango mkubwa wa mafanikio ya Morocco katika miaka ya hivi karibuni ni kiungo maarufu, Mohammed Khalid Timoumi, ambaye sasa ni mshauri mkuu wa kikosi cha Morocco kinachojiandaa kwa fainali za AFCON za mwaka ujao.
Katika miaka ya nyuma, kiungo alibaki muda mwingi katikati ya kiwanja, mshambuliaji aliganda mbele karibu na goli la wapinzani, hata timu ilipoelemewa na hakukaribia katikati ya kiwanja.
Miongoni mwa wachezaji wachache wa kiungo waliovuka mstari unaogawa kiwanja sehemu mbili ni Timoumi ambaye alichaguliwa kwa kura nyingi kuwa mchezaji bora wa soka wa Bara la Afrika wa 1985.
Mchezaji pekee wa Morocco aliyemtangulia kwa kupewa heshima hiyo ni Ahmed Faras katika mwaka 1975 na kufuatiwa baadaye na Badou Zaki (1986) na Mustapha Hadji (1998).
Timoumi mwenye urefu wa futi 6 na inchi 2 na mwili jumba, alilisakata kandanda kwa uhakika na kujiamini katika kiwango cha kitaifa na kimataifa kwa zaidi ya miaka 20. Kila umri wake ulipokuwa mkubwa alizidi kuwa imara.
Anakumbukwa alivyozichezesha mchakamchaka Ujerumani Magharibi, Ureno, Uingereza na Poland na kuiwezesha Morocco kuingia mzunguko wa pili wa fainali za Kombe la Dunia za 1986 zilizofanyika Mexico.
Morocco ilifungwa 1-0 na Ujerumani Magharibi katika mchezo wa kwanza, ikaichapa Ureno 3-1 na ikatoka suluhu na England.
Katika mchezo wao na Poland ilitoka suluhu na kusonga mbele na kuandika ukurasa mpya katika historia ya Kombe la Dunia kwa kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kuvuka mzunguko wa kwanza wa fainali za mashindano haya.
Akiwa kiungo na nahodha wa Morocco, Timoumi kamwe hatasahauliwa na Wareno kwa kufanya kazi kubwa iliyoshuhudiwa Abderrazik Khairi akifunga mabao mawili yaliyoiwezesha Morocco kuifunga Ureno 3-1. Matokeo ya mchezo ule yanahesabika hadi leo kama ni ya kihistoria.
Hadi leo wachezaji wa zamani wa Ureno husema hawaisahau siku ile waliyoiita ‘Siku Nyeusi’. Baada ya matokeo ya mchezo, magazeti ya Ureno yalikuja na vichwa vya habari kama “Huwezi kuamini, Ureno ipo kwenye msiba mkubwa” na ‘Masikini Ureno’.
Akizungumzia hivi karibuni tukio hilo la fainali za Kombe la Dunia za 1986, Timoumi alisema: “Tulipokuwa Mexico tulibeba mizigo mitatu na kila mmoja ulikuwa mzito, Kwanza ilikuwa kulinda heshima yetu kama wachezaji, pili kuiwakilisha Morocco na tatu kuonyesha wakati umepita wa kuidharau Afrika katika kandanda. Nashukuru tulifanikiwa.”
Mohamed Timoumi alizaliwa katika jiji la Rabat, Morocco, Januari 15, 1960. Baada ya kuchezea klabu za mtaani, alijiunga na klabu ya FAR iliyopo Rabat.
Alikaa nayo kwa zaidi ya miaka 10 na kuiwezesha mara nyingi kuwa klabu bingwa na alikuwamo katika kikosi cha Morocco kilichoshiriki mashindano ya Olimpiki ya 1984.
Akicheza kama kiungo, Timoumi alishirikiana vizuri na washambuliaji Abdelkarim ‘Fery’ Krimau na Bourdeballa na kipa Badou Zaki ambaye alichaguliwa na Shirikisho la Kandanda la Kimataita (FIFA) kuwa kipa bora wa Afrika wa karne iliyopita.
Kipa huyu alisifika kwa kuzuia makombora ambayo yalionekana hayawezi kuzuilika yasitikise nyavu za Morocco.
Timoumi pia alichezea klabu za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Lokeren ya Ubelgiji na Murcia ya Hispania katika nyakati tofauti.
Katika mwaka 2006 Shrikisho la Kandanda la Afrika (CAF) lilimchagua Timoumi kuwa mmoja wa wachezaji bora wa Bara hili katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.
Baada ya Morocco kushindwa kufaulu kuingia fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini na Kombe la AFCON zilizofanyika Angola miaka michache iliyopita Timoumi alisema inasikitisha kuona kiwango cha kandanda cha Morocco kimeshuka.
“Kwa kweli hii ni aibu na fedheha. Mataifa mengi ya Afrika yalikuwa yanatuheshimu na kutuogopa, lakini leo sisi ndio woga na hatujiamini,” aliongeza.
Kutokana na hali hii aliamua kufundisha kandanda wachezaji chipukizi wa kuanzia miaka 11 hadi 15 na anaamini pakifanywa juhudi za kutosha hali itarudi kama ilivyokuwa hapo zamani na kusema kinachohitajika ni mashirikiano na kujituma na sio kisingizio hiki na kile au kulaumiana.
Alitoa mfano wa klabu ya FAR Rabat aliyoichezea kwa muda mrefu kuwa iliweza kupata mafanikio makubwa kwa vile ililea vijana chipukizi ambao baadaye walipandishwa daraja baada ya kukomaa kimwili na umri.
Wachezaji hawa walicheza katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo na kuweza kuipatia mafanikio makubwa na nchi hapo baadaye.
Morocco leo ndiyo timu ya kwanza kutoka Afrika kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia, ilipofanya hivyo mwaka 2022 kule Qatar ambapo iliifunga Ureno 1-0 yenye mastaa kibao kama Cristiano Ronaldo, Bruno Fernandes, Bernardo Silva na wengineo, na kurudia historia ya kina Timoumi ya kuwafunga Wareno, lakini mara hii wakiandika historia kubwa zaidi.
Sasa tusubiri ushauri wake kwa timu ya Morocco inayojiandaa kwa AFCON hapo mwakani utazaa changa au mbivu.