Geita. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita imemhukumu kifungo cha miaka mitano jela Matokeo Petro (34), mkazi wa Bukombe mkoani Geita baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la jaribio la kutaka kumuua Josephat Mhozi (51).
Hukumu hiyo imetolewa leo Oktoba 2, 2024 na Jaji wa Mahakama hiyo, Athuman Matuma baada ya kuridhishwa na hoja zilizotolewa na pande zote mbili.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Matuma amesema ushahidi uliotolewa mahakamani hapo umeonyesha mwathirika wa tukio hilo, Mhozi, alipata mashambulizi mabaya ambayo yangeweza kusababisha kifo chake.
Jaji Matuma amesema licha ya maombolezo yaliyotolewa na wakili wa upande wa utetezi, Yisambi Siwale aliyetaka Mahakama imhurumie mteja wake kwa kuwa ni kijana mdogo ambaye Taifa linamtegemea, Jaji Matuma amesema hakubaliani na ombi hilo kwa kuwa Taifa haliwezi kutegemea wahalifu.
Kuhusu mshtakiwa kuwa na watoto na mke anayemtegemea, hawezi kumpa nafuu kwa kuwa wategemezi wake wanapaswa kuona kosa alilolitenda mshtakiwa ili nao wajifunze.
Jaji amekubaliana na ombi la Wakili Siwale aliloomba Mahakama izingatie muda wa miaka minne ambayo tayari mshtakiwa amekaa rumande na kusema kwa kosa hilo, adhabu ya juu kabisa ni kifungo cha maisha, hivyo kwa kuzingatia muda aliokaa rumande, Mahakama inamhukumu kwenda jela miaka mitano.
Mshtakiwa Matokeo alidaiwa kutenda kosa la kujaribu kuua kinyume na kifungu cha 211(a), sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2019.
Mshtakiwa huyo alijaribu kumuua Mhozi kwa kumpiga risasi kwa kutumia bunduki ya kienyeji maarufu kama gobore kwa kumshambulia kifuani upande wa kulia na kusababisha majeraha makubwa yaliyopelekea kuvuja damu nyingi na kumsababishia shida ya upumuaji.
Upande wa mashtaka katika kuthibitisha kosa hilo, ulikuwa na mashahidi wanne waliothibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wawili ambao katika ushahidi wao uligongana.
Siku ya tukio Novemba 10, 2020 katika Kijiji cha Nyamsega wilayani Bukombe, saa 4 usiku, mshtakiwa alidaiwa kumpiga risasi Mhozi wakati akitoka chooni.
Shahidi wa kwanza ambaye ni mwathirika wa tukio hilo, alidai alipotoka chooni akiwa anarudi ndani, alimuona Matokeo akiwa na gobore mkononi, alimwita na kumuuliza anafanya nini kwenye eneo hilo usiku huo na hakumjibu na ghafla alimpiga risasi upande wa kulia wa kifua na ikatokea mgongoni.
Alidai baada ya tukio hilo, alipiga kelele na mke wake kumfuata na kelele hizo zilizowaamsha majirani. Wakati akimfuata mumewe, alikutana na Matokeo na kumuuliza kwanini anamuua baba yake, hakumjibu kitu.
Shahidi huyo alidai kuwa kabla ya tukio hilo, yeye na mshtakiwa ambaye ni mtoto wa binamu yake, walikuwa na mgogoro uliotokana na yeye (Josephat) kununua mizinga ya nyuki iliyoachwa na mjomba wake (babu yake Matokeo) ambayo mshtakiwa alikuwa akiitunza.
Shahidi mwingine ambaye ni daktari aliyempokea Josephat na kumpatia huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa Hospitali ya Kanda Bugando, alieleza kuwa akiwa zamu usiku, alimpokea mgonjwa akilalamika kifua kubana huku akivuja damu kifuani na alikuwa na jeraha kama la kitu butu kuingia ndani.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya daktari wa Bugando aliyefanya X-ray, pafu la upande wa kulia lilikuwa limejaa damu na kuna kidude cha chuma kilichokuwa kwenye mapafu.
Akitoa utetezi wake mahakamani hapo, Matokeo alidai siku ya tukio akiwa nyumbani amelala, mkewe alimwamsha akimwambia nje kuna kelele na waliposikiliza waligundua zinatokea kwa jirani yao ambaye ni Mhozi.
Alidai baadaye alitoka kwenda zilipokuwa kelele na kuhoji kilichotokea na kuelezwa baba yake amepigwa risasi na tayari amekimbizwa hospitali na kubaki eneo la tukio hadi asubuhi ya siku iliyofuata.
Amesema baada ya siku tano, alikamatwa na polisi akituhumiwa kuhusika na jaribio la kumuua Mhozi na kudai hakuwahi kuwa na mgogoro na mwathirika huyo wala hajawahi kumiliki silaha.
Shahidi mwingine wa utetezi, Anastazia William ambaye ni mke wa Matokeo, alidai alisikia kelele za mwano na kumwamsha mumewe ambaye alitoka na kwenda kwenye tukio lakini baadaye alirudi akidai Mhozi amepigwa bunduki.
“Alilala na kusema asubuhi ataamka aende kwa kuwa anajisikia kuumwa na asubuhi ya siku iliyofuata waliungana wote wawili, saa 12 asubuhi, kwenda nyumbani kwa Josephat,” amesema Anastazia.
Jaji Matema amesema katika makosa ya jinai upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha pasi kuacha shaka na katika shauri hilo hakuna ubishi kuwa Mhozi alijeruhiwa kama ushahidi wa upande wa mashtaka ulivyoeleza pamoja na kielelezo cha PF3 kilichotolewa mahakamani.
Amesema katika kesi hiyo, hoja bishaniwa ni nani alimshambulia mwathirika na upande wa mashtaka unadai ni mshtakiwa huku utetezi ukipinga.
Amesema upande wa mashtaka, shahidi wa kwanza na wa pili walimtambua mshtakiwa ambao wameeleza mtuhumiwa hakuwa mgeni kwao na ni mtoto aliyezaliwa na binamu lakini pia ni jirani yao.
Mashahidi hao wawili walieleza kumtambua kwa msaada wa taa ya sola na walikuwa karibu na mshtakiwa.
Kwa upande wa utetezi, walijitetea kuwa mshtakiwa amekamatwa siku tano baada ya tukio na katika ushahidi wake alidai walikamatwa wengine wawili lakini ushahidi ambao ulikuwa wa kusikia na sio wa kuona.
Tofauti na upande wa mashtaka ambao ushahidi wao uliendana, ushahidi wa upande wa utetezi uligongana wakati ambao mshtakiwa akidai alilala kwenye eneo la tukio hadi siku iliyofuata, mke wake alidai alifika kwenye tukio na kurudi nyumbani kwa kuwa alikuwa hajisikii vizuri.