Yanga yapokea ofa mbili za Mzize Ulaya

UONGOZI wa Klabu ya Yanga umethibitisha kupokea ofa kutoka katika timu za Ulaya ambazo zinataka kumnunua mshambuliaji Clement Mzize. 

Ingawa hakuwa tayari kuzitaja timu ambazo zinamtaka mchezaji huyo, lakini Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema mbali na Azam FC wamepokea ofa kutoka timu ambayo inashiriki Ligi Kuu Russia na nyingine ya Israel. 

“Ni kweli tumepokea ofa kwa ajili ya mchezaji wetu Mzize, kwasasa bado tupo kwenye mazungumzo hivyo sio vyema kuweka wazi kila kitu lakini mtambue tu timu ambazo zinamuhitaji ni kutoka Urusi na Israel,” amesema. 

Mzize ni zao la Klabu ya Yanga, ambaye kwa mara ya kwanza alipandishwa kutoka timu ya U-20 katika msimu wa 2021-2022 wakati huo ikiwa chini ya kocha Mwinyi Zahera.

Lakini, msimu huu baada ya kuondoka Fiston Mayele, Mzize amekuwa katika wakati mzuri akipata nafasi kubwa ya kucheza chini ya Kocha Miguel Gamondi ambapo hadi sasa amefunga mabao 10 kwenye michuano yote.

Kamwe amesema mbali na mataifa hayo kutoka Ulaya kumtaka Mzize lakini wamekuwa wakipata hodi kutoka kwa baadhi ya timu za barani Afrika ambazo zimekuwa zikiulizia wachezaji wao kadhaa kwa ajili ya kutaka kuwasajili. 

Ameongeza kwa kusema hiyo kwao haiwapi shida kwakuwa wanajua kuwa ni kutokana na ubora wa kikosi chao ndio maana hodi zimekuwa nyingi. 

Msimu uliopita akiwa chini ya kocha Nasreddine Nabi kwenye ligi msimu uliopita alifunga mabao matano na kutoa asisti moja, huku michuano ya kimataifa msimu huo amefunga mabao mawili dhidi ya Al Merrikh kwenye Uwanja wa Pele jijini Kigali ushindi ulioifanya Yanga kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mapema wiki hii Rais wa Yanga, Hersi Said alinukuliwa na moja ya chombo cha habari jijini Dar es Salaam akikiri kuwa hawatakuwa na chaguo la kumlazimisha mchezaji kubaki kwenye timu yao kama atakuwa haitaki kuendelea kuwapo. 

“Kuelekea dirisha la usajili tuna kanuni tatu, kushawishi wachezaji wabaki, kama itashindikana basi ni kuangalia ofa nzuri na mwisho ni kusajili mbadala sahihi,” amesema Hersi.

Related Posts