Pemba. Watu wawili akiwemo mwalimu wa Shule ya Msingi Finya wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa kutokana na ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Kinazini Wingwi Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Daktari wa Hospitali ya Micheweni, Hamad Mbwana Shoka ameieleza Mwananchi Digital leo Oktoba 2, 2024 kwamba wamepokea watu saba ambapo kati ya hao, wawili walikuwa wameshafariki dunia.
Amewataja waliofariki dunia ni Mohina Egland Nundu (38) mkazi wa Tanga ambaye ni fundi ujenzi katika Skuli ya Simai Micheweni na mwingine Safia Mohamed Yusuf (45) Mwalimu wa skuli ya Finya ambao wote pamoja na majeruhi waligongwa na gari baada ya kukosa mwelekeo barabarani.
‘’Tulipokea watu hao saa 7:00 mchana huku wawili hao wakiwa wamefariki dunia na katika uchunguzi wetu tulibaini waliumia sehemu za kichwani na wengine sehemu za miili yao,” amesema daktari huyo.
Kaimu kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mussa Mwakasula amethibitisha kutokea ajali hiyo ya gari ya kampuni ya ujenzi wa barabara IRIS baada ya kuacha njia na kuwafuata watu waliokuwa kando ya barabara wakisubiri usafiri.
Amesema Jeshi la Polisi linachunguza chanzo cha ajali hiyo huku akiwataka madereva kufuata sheria za barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.
‘’Nikweli watu wawili wamefariki dunia na wengine wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo baada ya gari ya Kampuni ya IRIS kuacha njia na kupoteza maisha ya watu hao na wengine kujeruhiwa,’’ amesema.
Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba, Mohamed Nasor Salum amesema wizara imeguswa na kifo cha mtendaji wao na kueleza kuwa ameacha pengo kubwa kutokana na juhudi alizokuwa nazo katika kuiletea matokeo mazuri skuli hiyo.
‘’Tumeguswa na kifo cha mtendaji wetu Safia Mohamed na fundi wa ujenzi wa skuli hiyo anatokea Tanga, Mwalimu huyo ameacha pengo kubwa kutokana na matokeo mazuri yanayopatikana katika skuli yake,” amesema.
Ameitaka familia ya marehemu kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba kwani yote hayo ni mipango ya Mwenyezi Mungu.