Tanesco yaibuka mshindi wa kwanza maonesho ya TIMEXPO 2024

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Ubunifu na Muonekano mzuri wa banda katika Maonesho ya Pili ya Kimataifa ya Viwanda Tanzania (TIMEXPO 2024).

Tanesco imekabidhiwa tuzo hiyo ya ushindi leo Oktoba 2,2024 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, wakati wa kufunga maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere (Sabasaba).

Waziri Jafo amesema jukumu kubwa la Serikali ni kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa viwanda kufanya uzalishaji, hivyo Serikali inafanya jitihada kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha nchini.

Amesema ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme wa Maji la Julius Nyerere utakapokamilika utawezesha upatikanaji wa megawati 2115 ambapo hadi sasa tayari megawati 705 zimeshaingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Amesema kwa sasa umeme unaozalishwa unawezesha viwanda kufanya shughuli za uzalishaji bidhaa bila vikwazo.

Wakizungumza kufuatia ushindi huo, watumishi wa Tanesco wamesema Tuzo ya Ubunifu na Muonekano Mzuri wa Banda waliyoipata katika maonesho hayo imewapa nguvu ya kujituma zaidi katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.

Maonesho hayo yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) wakishirikiana na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) yamehudhuriwa na wafanyabiashara mbalimbali, makampuni ya biashara kutoka ndani na nje ya nchi, taasisi za umma, binafsi na taasisi za fedha.

Maonesho hayo yaliyoanza Septemba 26,2024 yamewakutanisha pamoja wafanyabiashara mbalimbali pamoja na taasisi za fedha kwa lengo la kukuza biashara na kujenga ushirikiano.

Related Posts