MLANDIZI Queens ni miongoni mwa timu zenye umaarufu na historia kubwa nchini mbali ya Simba Queens na Yanga Princess, ikiwa imeshatwaa ubingwa wa Tanzania msimu wa 2016/17 na kutoa wachezaji mahiri akiwamo Mwanahamis Omary ‘Gaucho’, Donisia Minja na Asha Mwalala.
Mlandizi wanarudi Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) baada ya misimu miwili tangu waliposhuka daraja mwaka 2022.
Timu hiyo yenye makao makuu Mlandizi mkoani Pwani imetengeneza kikosi chini ya kocha mkuu, Jamila Kassim huku ikitengeneza kikosi cha wachezaji 26 wakiwamo wapya na wale wa zamani.
Kocha wa timu hiyo, Jamila Kassim aliliambia Mwanaspoti, malengo yao kwanza ni kutengeneza kikosi ambacho kitakuja kuwa na ushindani na msimu unaofuata ndiyo watafikiria ubingwa.
Jamila aliongeza, wamekaa nje bila kucheza Ligi Kuu kwa muda mrefu akiamini wamejifunza kitu na sasa wanarudi kwa kishindo.
“Kama mnavyojua sisi ndio tumeweka rekodi ya kwanza ya kuchukua ubingwa, kwangu pia natamani kama kocha niiweke rekodi hiyo, ingawa msimu huu tunataka kutengeneza kikosi cha kina Mwanahamis Omary ‘Gaucho’ wengine wengi,” alisema Jamila na kuongeza;
“Pre-season yetu tayari tumecheza mechi ya kirafiki kubwa na Yanga Princess tukafungwa lakini ilikuwa kipimo kizuri kwetu.
“Mlandizi tunaweza kusema ni kama ngeni kwa sababu imepita misimu miwili bila ya kuonja Ligi Kuu, ni mtihani mkubwa na ni ngumu kwahiyo tunapaswa kuwa makini tuwe na timu ya kushindana na tucheze soka la kisasa ili tuibakishe timu katika Ligi Kuu,”
Ofisa Habari wa timu hiyo, Sajida Sadick anasema kama viongozi watahakikisha kila jambo linakwenda sawa ili kutengeneza kikosi bora ambacho kitakuwa tishio.
“Malengo ya klabu ni kutengeneza timu kisha tusalie ndani ya nafasi nne za juu lakini kama tutafanikiwa hilo na zaidi tuchukue ubingwa japo haitakuwa rahisi lazima tujitoe kwelikweli.”
Mdau wa soka la wanawake, Victoria Mungure anasema kama wanataka kurudia rekodi yao basi wahakikishe wanajipanga kwa kuwa ligi imebadilika.
“Kila timu iliyopo Ligi kuu imejipanga kuanzia usajili, maandalizi hata kambi zao kwa hiyo wanapaswa kujipanga haswa, nimeona wamecheza mechi za kirafiki hizo ndio za kujitathmini,” alisema Mungure na kuongeza:
“Lakini hata kwa mkoa wa Pwani wanaisaidiaje timu yao kwa kuipa sapoti timu hiyo, pia wadhamini wajitokeze kuunga mkono timu za wanawake kwani sasa hivi michezo ni ajira kubwa, soka la wanawake linakua kwa kasi, tazama kuna wachezaji wanacheza ligi kubwa kina Aisha Masaka, Clara Luvanga na wengine.”
Kocha wa zamani wa Geita Queens iliyoshuka daraja, Sultan Juma alisema ili kuirudisha Mlandizi yenye ushindani inahitaji maandalizi mazuri, bajeti na kusajili wachezaji wazuri.
“Kama wameandaa timu vizuri, wamesajili wachezaji kwa kuwa wale waliotoka nao daraja la kwanza sio wabaya lakini unahitaji kuongeza wenye ushindani, makocha pia ambao watakuwa wanaelewana na viongozi,” alisema Juma.
Mdau wa soka jijini Pwani, Mwanahamis Abdallah anashauri timu hiyo kusajili wachezaji, makocha na benchi la ufundi ambalo lina uzoefu kwenye ligi hiyo.
“Tumekaa muda mrefu bila kushuhudia burudani ya soka na kwa hapa Pwani, Mlandizi ndio timu pekee hivyo tunawaomba viongozi waweke mipango mizuri sio leo unapanda ligi kesho tena unashuka,” anasema Mwanahamis.