Mchengerwa aagiza mchakato uanze  kuipandisha hadhi Wilaya ya Arusha

Arusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Arusha kuanza mchakato wa kuomba kuipandishwa hadhi Halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuwa Halmashauri ya Mji wa Arusha.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 2, 2024 wakati akizungumza kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuwasilisha ombi la halmashauri hiyo kupandishwa hadhi.

Mchengerwa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Mussa kwa kushirikiana na uongozi wa wilaya, kuanza mchakato kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na wakijiridhisha wapeleke Tamisemi kwa ajili ya kupelekwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nawaagiza Katibu Tawala wa Mkoa na Wilaya, mchakato huo uanzie kwenye wilaya uende kwenye RCC halafu mkoa utatuletea Tamisemi na tukijiridhisha vigezo vimetimia, tutapeleka kwa Rais ipandishwe hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji,” amesema.

“Anzeni mchakato ili vigezo vilivyowekwa kisheria kama mmekidhi tupeleke kwa Rais. Dhamira ya Rais ni miji ambayo imeshakua kuikuza zaidi kuimarisha mamlaka ya utawala katika miji ili wananchi wasogezewe huduma,” ameongeza.

Kuhusu barabara, amesema atawasiliana na Wakala wa Huduma wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ili barabara zinazohitaji udharura zifanyiwe marekebisho, zipitike msimu wote wa mwaka.

“Tutapita huko kujionea na kwa kuwa Tarura tutazingalia kwa sababu fedha za dharura zipo na kwa kuwa bajeti kutoka Sh250 bilioni hadi Sh1.5 trilioni,” amesema.

Awali, Makonda aliwasilisha maombi mawili ambapo la kwanza alieleza kuwa Wilaya ya Arumeru ni moja ya wilaya zenye barabara mbovu.

“Moja ya wilaya ambayo inahitaji msaada na jicho la kipekee upande wa barabara ni wilaya hii ambayo ina halmashauri mbili na kwa namna ya kipekee barabara hizi ziko ambazo zinaenda kwenye kuchochea maendeleo ya wananchi na zikijengwa zitaongeza uchumi,” amesema.

Makonda amesema walifanya ziara na timu ya mkoa na miongoni mwa malalamiko waliyopokea ni pamoja na ya migogoro ya ardhi kuibuka katika mamlaka ya mji mdogo.

“Halmashauri ya Wilaya ya Arusha wanatamani kama Arusha tuna Jiji, basi na wao wapandishwe hadhi kuwa manispaa,” amesema Makonda.

Related Posts