BASHE: MADIWANI SIMAMIENI VYAMA VYA MSINGI VISIWADHULUMU WAKULIMA


MADIWANI wa Kata ya Chiwale, Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara wameelekezwa kusimamia Vyama vya Msingi vya Ushirika ili visiwadhulumu wakulima kwa kuwa ndiyo msingi wa mapato ya kuviendesha vyama hivyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo tarehe 2 Oktoba 2024 ambapo amewakumbusha Madiwani dhana ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuwa na ushirika imara wa vyama kwa maslahi mapana ya wakulima.

Waziri Bashe alionekana kusikitishwa na mmoja wa Madiwani ambaye aliwahi kuwa Katibu wa Nanyindwa AMCOS, ambacho ni chama chenye madeni ya zaidi ya shilingi milioni 139 za wakulima. “Nyinyi ni wasimamizi wa wananchi, simamieni vyama vya msingi ili visiwadhulumu wananchi. Hatuwezi kuwa na viongozi wa namna hii, siyo sawa,” amekemea Waziri Bashe.

Aidha, amewatia moyo wakulima kwa kuwaambia mambo makuu matano: (1) malipo wakati wa msimu wa korosho unaoanza hivi karibuni yatalipwa kupitia mfumo wa TMX ambapo Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU kitalipwa ili kiwalipe moja kwa moja wakulima; (2) Minada ya mbaazi haitofungwa muda ukifika bali itahamishiwa kuendelea kwenye mnada wa Korosho ili wakulima wa mbaazi waendelee kuuza; (3) kila mkulima awe na akaunti ya benki ili kulinda haki za malipo. Aidha, Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Bw. Nyagiro ameelekezwa kuhakikisha benki za NMB, CRDB na NBC zinawafikia wakulima.

Jambo la nne limeelezwa kuwa programu ya BBT Korosho inaanzishwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) ambapo Maafisa Ugani 500 wataajiriwa na Bodi ya Korosho kutoa huduma za Ugani vijijini, usajili na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima. Na mwisho, Waziri Bashe amewaeleza wananchi hao kuwa Wizara italeta wataalamu watakaopita kwenye Vijiji kutathmini hali ya uzalishaji, vyama vya AMCOS na kubaini uhalisia wa huduma za vyama na uzalishaji unaopatikana.

“Nisisitize kwa wakulima kuwa nyie ndiyo mnaohalalisha uwepo wa hivi Vyama vya Msingi kutokana na makato mnayokatwa. Hivyo, makato mnayokatwa mnapouza mazao ni uhalali wa haki ya uanachama. Haki yako ni ya kuchagua Chama au kuchaguliwa ndani ya Chama,” amesema Waziri Bashe.


Related Posts