Serikali yaangukiwa kukiongezea bajeti kitengo cha elimu ya watu wazima

Serikali imetakiwa kuongeza bajeti kwa ajili ya kitengo cha elimu ya watu wazima ili kuboresha na kuongeza ufanisi kwenye kitengo hicho ambacho kimekuwa na msaada mkubwa katika kuongeza uelewa kwa wanafunzi waliocheleweshwa kujiunga na masomo kwa njia ya mfumo rasmi.

Wito huo umetolewa na Yusuph Yahaya ambaye ni afisa taaluma sekondari wilaya ya Wanging’ombe wakati wa maadhimisho ya juma la elimu ya watu wazima wilaya ya Wanging’ombe yaliyofanyika katika kata ya Ilembula wilayani humo.

“Ili mpango wa elimu ya watu wazima uweze kuboreshwa zaidi,kitengo kinashughulika na programu nyingi hivyo tunaomba kwa mwaka wa fedha 2024 – 2025 kitengo kitengewe bajeti ya kutosha na walimu wanaofundisha madarasa ya memkwa wapewe mafunzo ya mara kwa mara ili kuhusisha taarifa zao”amesema Yahaya

Yahaya amesema ili kuongeza fursa ya wanafunzi walioshindwa kujiunga katika elimu ya msingi na sekondari katika wilaya hiyo ameiomba halmashauri itenge shule mbili za msinngi pamoja na shule moja ya sekondari zitakazoongezewa miundombinu kwa ajili ya wanafunzi watakaosoma masomo ya ufundi.

Damasi Kavindi ni afisa tarafa ya Wanging’ombe,kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo amewataka wananchi kuhamasisha maendeleo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na kumuagiza mkurugenzi kuhakikisha anatenga bajeti za ndani kwa ajili ya kitengo hicho.

“Mkurugenzi hakikisheni mnatenga bajeti katika bajeti zenu kwa ajili ya mipango mbalimbali ya elimu ya watu wazima ili kuhakikisha kitengo kinafanya kazi bila kuyumba”amesema Kavindi

Baadhi ya wazazi akiwemo Patrick Kitalima wanasema elimu ya watu wazima imekuwa na umuhimu mkubwa hususani kwa watu waliokosa fursa ya kupata elimu wakati wakiwa na umri mdogo na kuiomba serikali kuendelea kuboresha mfumo huo kwa ajili ya kujenga kizazi chenye uelewa.

Mariano Mhule na Nuru Mkenja ni baadhi ya wanafunzi kutoka shule ya msingi Igelehedza wanaishukuru serikali kwa mpango huo wa kutoa elimu kutokana msaada mkubwa wanaopata ili kuongeza maarifa bila ubaguzi.

“Wanafunzi wa elimu ya watu wazima hatujatengwa wala hatubaguliwi tunamshukuru sana Rais wetu kwa kuwa ningekuwa sisomi ina maana ningekuwa mtaani bila elimu yeyote ni naomba wazazi waendelea kutoa nafasi kwa watoto ili waweze kwenda shuleni”amesema Mariano

Related Posts