Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura Hospitali ya Benjamini Mkapa Dkt. George Dilunga ametoa rai kwa wanafunzi wanaopata nafasi ya kupata Mafunzo ya kutoa Huduma ya Dharura kutumia vizuri elimu wanayopata katika kuhudumia wagonjwa.
Kauli hiyo imetolewa wakati Ujumbe wa Abbott Fund uliongozwa Mkurugenzi wake Robert Ford uliotembelea kujionea miradi mbalimbali ya afya inayotekelezwa na Abbott fund ikiwemo Kituo cha Kutoa Mafunzo ya Huduma ya Dharura kilichopo Hospitali ya Benjamini Mkapa kinachohudumia Mikoa ya Kanda ya Kati Mikoa ya Dodoma Tabora Singida Manyara na Iringa.
Ameongeza kusema kituo hicho cha Kutoa Mafunzo Huduma za Dharura kimejiwekea mipango ya kufanya mafunzo kwa kila mwezi awamu mbili, ambapo kila awamu kitakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 20 hivyo kujiwekea malengo ya kufanya mafunzo kwa wanafunzi 40.
Dkt Dilunga Amesema, “tumelenga kuwapatia mafunzo ya huduma kwa wale wanafunzi waliopo kazini na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ili kuwajenga uwezo mzuri wa kuwapa huduma wagonjwa wetu”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Benjamini Mkapa Dkt. Kessy Shija amemshukuru Mwenyekiti wa Abbott Fund kwa kutembelea mradi huo ambao ujenzi na vifaa ulifadhiliwa na Mfuko huo.
“Tunamshukru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kuwa na Vituo vya Kutoa mafunzo ya Huduma Dharura ili kutoa mafunzo kwa watoa huduma na kuboresha huduma za dharura,” alisema Dkt, Shija.
Aidha tumelenga kutoa mafunzo mpaka katika ngazi zote ikijumuisha ngazi ya Hospitali za Kanda Hospitali za Mkoa, Hospitali za Wilaya Vituo vya Afya na Dispensari na matarajio yetu ni kwamba mafunzo haya yatakuwa na manufaa kwa Nchi yetu na kwa jamii yetu.
Naye Mtendaji Mkuu (CEO) wa Shirika la Abbot Fund, Robert Ford, ameridhidhishwa na utekelezaji wa mradi wa maabara ya ujuzi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).
Ford, ameahidi kuwa Abbot Fund itaendelea na ushirikiano na BMH.
“Hii ni Hospitali namba moja hapa Dodoma. Inabidi mjivunie kuwa na kuwa na hii Hospitali,” amesema C.E.O wa Abbot Fund wakati wa ziara yake BMH.
Shirika la Abbot Fund waligharamia ujenzi wa maabara ya ujuzi ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa thamani ya 400m/-. Maabara hii imezinduliwa na Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, mwezi Septemba.