Kwa miezi kadhaa baada ya wanamgambo wenye itikadi kali kufanya mashambulizi huko Kafolo kaskazini mwa Ivory Coast mwaka 2020, mji huo ulitelekezwa. Miaka minne baadaye umeanza kustawi na hii ni kutokana na mpango wa muda mrefu wa serikali wa kuongeza ulinzi, kupambana na umasikini na kukabiliana na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Juni 2020, wanajeshi 14 waliuwawa katika shambulio la awali na kisha wengine wawili waliuwawa mwezi Machi mwaka uliofuata. Kilichofuata ni kuwa mji wa Kafolo ulikimbiwa, na maduka yalifungwa. Wakaazi wake walijificha kwenye kaya zao wakihofia mashambulizi zaidi.
Hivi sasa mji huo umeanza kuwa na watu. Migahawa, huduma za kutengeneza nywele na karakana za magari zimefunguliwa huku wakaazi wakiendelea na maisha yao kama kawaida. Chifu wa eneo hilo Tiemogo Bamba anasema kumekuwa na mabadiliko mazuri na vijana wanahusishwa kuendeleza kijiji. Mamlaka zimeshaweka maeneo kwa ajili ya mafunzo na semina.
Soma pia: Ouattara ashinda muhula wa tatu Cote d’Ivoire kwa kishindo
Mwanzoni mwa mwaka 2022, mamlaka za taifa hilo lililo magharibi mwa Afrika lilizindua programu ya vijana iliyolenga hasa mikoa ya kaskazini inayopakana na Burkina Faso na Mali, mahali ambako makundi kadhaa ya wabeba silaha yanafanya operesheni zao.
Madhumuni ya programu hizo ni kuhakikisha kuwa vijana wanajifunza biashara ili wasishawishike kujiunga na makundi ya wanamgambo na wachimbaji haramu wa madini ambao huwachukua watu kutoka eneo hilo.
Kambile Koko ni mmoja wa vijana wanaopatiwa mafunzo ya uhunzi kwenye mji huo mdogo. Anasema kujifunza ujuzi wa aina fulani ni bora kuliko kuzurura bila kazi. Anaongeza kuwa mtu akikaa bila kazi ni rahisi kushawishika ikiwa mtu mwingine atakuja na kumpa fedha na pikipiki ili akafanye shughuli za kihalifu
Kila mwezi anapata karibu dola 50 kutoka serikalini kama sehemu ya mpango wa kusaidia mafunzo yake. Kupitia fedha hizo anabainisha kuwa anaweza kujinunulia chochote na kula na hilo linamuhamasisha kujifunza biashara. Vijana wengine wa Kafolo wamepewa mikopo.
Shirika la habari la Ufaransa, AFP lilipoutembelea mji huo mwezi Septemba, Chifu Tiemogo Bamba wa eneo hilo hakuwa na wasiwasi na mashambulizi bali mafuriko ambayo yamezimeza baadhi ya nyumba tangu Mto Comoe ulipofurika na kingo zake zikapasuka.
Soma pia:Cote d’Ivoire yaanza mazungumzo na wanajeshi
Bamba anaeleza kuwa kwa sasa kuna wanajeshi wengi na watu hawaogopi kuanza kulima tena. Hata hivyo, bado wana wasiwasi kutokana na ukosefu wa usalama unaoendelea katika upande wa Burkina Faso.
Uhusiano wa kidiplomasia uliojawa na mivutano kati ya serikali ya Ivory Coast na watawala wa kijeshi wa Burkina Faso umeendelea kusababisha ugumu kwa watu kufanya shughuli zao mpakani.
Mfanyabiashara Naminata Bamba aliyetumia mkopo aliopewa na serikali kufungua tena mgahawa wake anasema awali walikuwa na soko siku tano za wiki. Watu kutoka Burkina Faso walifika Kafolo na walinunua bidhaa zao, lakini kwa sasa bado kuna hofu, na hilo haliwezekani tena.
Anaongeza kusema kuwa wafanyabiashara wanahofia kuvuka mpaka kwenda upande wa pili kutokana na makundi ya wanamgambo pamoja na wapiganaji waliojitolea kujiunga na jeshi la Burkina Faso ili kuimarisha ulinzi ambao wanatuhumiwa kufanya udhalilishaji dhidi ya raia.