NMB yazindua akaunti ya Kikundi

Benki ya NMB imezindua akaunti ya kikundi yenye  maboresho makubwa kwa wanakikundi wote kufurahia huduma kidijitali. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Uzinduzi huo umefanyika leo Ijumaa mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima na kuhudhuriwa na wanavikundi zaidi ya 400.

Akizungumzia akaunti hiyo Afisa Mtendaji Mkuu, Ruth Zaipuna amesema akaunti hiyo imetokana na maboresho yaliyotokana na mrejesho wa wanachama wa vikundi 200,000 vyenye wanachama zaidi ya milioni moja wa iliyokuwa NMB Pamoja Akaunti.

NMB Pamoja akaunti ilizinduliwa mwaka 2020 na sasa  imekuwa NMB Kikundi Akaunti ambayo imezinduliwa leo na kuifanya kuwa akaunti ya kidigitali yenye unafuu, urahisi na usalama katika matumizi yake.

“Ni kutokana na mabadiliko na maboresho hayo, kila mwanakikundi sasa anaweza Kuteleza Kidijitali na NMB Kikundi Akaunti, ikiwemo kufungua akaunti papo hapo, kuchangia michango na kukopeshana mikopo ya kikundi, kuhamisha fedha kwa wanakikundi bila makato na kupata taarifa za kikundi kwa uwazi, na usalama wakati wote, mahali popote.

“Aidha, NMB Kikundi Akaunti itawawezesha wanakikundi kuchangia michango ya kikundi bila haja ya vikao wala kutembelea tawi la NMB, kuangalia salio na taarifa fupi ya kifedha ya kikundi, kubwa zaidi akaunti hii inajumuisha Bima ya Maisha, ikiwapa wanakikundi uhakika wa kifedha na amani ya akili kwa mwanachama na familia yake,” amefafanua Zaipuna.

Kutokana mafanikio hayo, Dk. Gwajima ameipongeza menejimenti na wafanyakazi wa NMB kwa kuja na NMB Kikundi Akaunti, ambayo ni suluhisho kubwa na mbadala katika utoaji huduma jumuishi za kifedha kwa vikundi vya kijamii vya kuweka akiba na kukopa.

Amesema ujio wa akaunti hiyo, ni zaidi ya ubunifu katika ustawi na maendeleo ya vikundi na wanachama wake.

“NMB Kikundi Akaunti ni jitihada za wazi za Benki ya NMB katika kusapoti juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imejikita katika kutekeleza mpango wa taifa wa huduma jumuishi za kifedha ili kuhakikisha idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki inaongezeka maradufu.

“Kwa hiyo kuboreshwa na hatimaye kuzinduliwa kwa NMB Kikundi Akaunti – ambayo ni ya pamoja kwa wanachama wa vikundi, ni utekelezaji wa malengo na mkakati wa serikali ya Rais Samia ya kuongeza ujumuishwaji wanawake na makundi mengine kwenye hduma jumuishi za kifedha na kubwa zaidi usalama wa fedha zao,” amesema na kuongeza;

“Imeelezwa hapa kuwa NMB Kikundi Akaunti tunayoizindua leo sio tu suluhishi ya changamoto mbalimbali za vikundi vya kijamii, bali pia imebeba huduma ya Bima ya Maisha kwa wanakikundi am,bao sio lazima wawe na akaunti binafsi ya NMB, hili jambo jema na la kibunifu linaloakisi dhamira njema ya benki kwa jamii.”

Kupitia akaunti hiyo, wanakikundi wataweza kutumia NMB Mkononi, kufungua akaunti kiurahisi na papo hapo kwa kubofya *150*66#, kuchangia michango na kukopeshana mikopo ya kikundi kupitia simu zao na kuhamisha fedha kwa wanakikundi bila makato yoyote.

Related Posts