Na Chalila Kibuda,Michuzi TV Zanzibar
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) Dkt. Redempta Mbatia amesema Tanzania inakabiliwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza, huku kukiwa na ongezeko la magonjwa ya kuambukiza, ikiwa ni pamoja na VVU, Kifua Kikuu na magonjwa mengine ya mlipuko.
Dkt.Mbatia aliyasema hayo katika Jukwaa la Afya katika mkutano wa 11 wadau wa Afya Tanzania (THS) lililondaliwa na THPS kwa kushirikiana na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (US. CDC) lilofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Zanzibar (ZITF).
Alisema jukwaa hilo lililenga kujadili namna nzuri ya kushughurikia magonjwa hayo katika kipindi ambacho bajeti ya afya nchini bado ni ndogo na pia katika miaka ya hivi karibuni hata ufadhili wa afua za afya umekuwa ukipungua kwa kiasi kikubwa.
Kwahiyo ni muhimu kwa sekta ya umma, kwa kushirikiana na asasi zisizo za kiserikali na sekta binafsi ili kuwekeza katika kinja na utoaji wa huduma za afya jumuishi.
Dkt. Mbatia alizumumzia uzoefu wa Shirika ya THPS katika kutoa huduma jumuishi za magonjwa yasiyoambukiza katika kliniki za tiba na matunzo za VVU nchini kwa kipindi cha Machi 2023 hadi Agosti 2024.
Aliongeza kuwa THPS inalenga katika kushughulikia changamoto mbalimbali za afya ya umma, ikiwa ni pamoja na VVU na UKIMWI, kifua kikuu, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana, maabara na mifumo ya taarifa za usimamizi wa afya, UVIKO- 19, na tathmini za afya ya umma.
Amesema mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021- Septemba, 2026)
Kupitia mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua ambao unatekelezwa katika mikoa minne ya Tanzania: Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga, THPS imekuwa ikitoa huduma za kinga, matunzo, na matibabu ya VVU, ikijumuisha Tohara Kinga kwa wanaume (VMMC) katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga, na Mpango wa DREAMS mkoani Shinyanga.
Mpango wa DREAMS ni mpango wa ambao unalenga wasichana rika balehe na wamama wadogo kwa ajili ya kuwapatiz huduma mbalimbali za VVU.
Jukwaa hilo lilijikita kwenye mada “Ushirikiano wa Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi katika huduma endelevu za kinga na matunzo katika kushughulikia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.”
“Athari zinazohusiana na magonjwa yasiyoambukiza zinaongezeka kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha na gharama kubwa za huduma ya afya kwa magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na upungufu wa rasilimali ndani ya bajeti ya sekta ya afya na kupungua kwa ufadhili inabidi mtazamo wetu ujikite zaidi katika kuzuia magonjwa na kuunganisha huduma zenye gharama nafuu “amesema Dkt.Mbatia
Aidha Jukwaa hilo lililenga kuwaleta pamoja wataalam ili kujadili mikakati endelevu ya kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya kuambukiza nchini Tanzania kwa kutumia rasilimali zilizopo.
“Ujumuishaji wa huduma bora wa huduma za uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu ndani ya huduma za VVU utaimarisha afya za wapokea huduma za tiba na matunzo, ubora na huduma zinazomlenga mtu binafsi na kupelekea kupata huduma za afya zilizo endelevu na thabiti.” Alisema Dkt. George S. Mgomella Mkurugenzi wa Miradi CDC Tanzania.
Nae Mkurugenzi Mtendaji na daktari mshauri katika Hospitali ya Shree Hindu Mandal jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Kisukari Prof. Kaushik Ramaiya alitoa wasilisho kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na kupendekeza uundaji wa muundo jumuishi wa huduma za matunzo ya magonjwa sugu.
Amesema wagonjwa wakipata huduma jumuishi kutapunguza vifo vya wenye ukimwi kutokana kudhibiti mapema kwa magonjwa yasioambukiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ndogo ya matibabu kupitia ima Tanzania Dkt. Ismail Gatalya, ambaye aliwasilisha mada kuhusu rasilimali fedha za afya kwa utaratibu wa bima unaozingatia magonjwa yasiyoambukiza.
Meneja Programu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) Dkt.Prosper Faustine aliwasilisha mada kuhusu mafanikio na changamoto wanazopitia wapokea huduma za tiba na matunzo ya VVU wenye umri mkubwa,
Daktari Bingwa wa Hospitali ya Kibong’oto, Prof. Stella Mpagama akijadili kuhusu ujumuishaji wa matokeo ya utafiti wa magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kwa vitendo katika mifumo ya utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania.