TCU yafungua dirisha jipya udahili elimu ya juu

 

Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), imefungua awamu ya tatu ya udahili wa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na elimu ya juu, kutuma maombi ndani ya siku tano (5), kuanzia kesho. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam  (endelea).

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa, ametangaza kufunguliwa kwa awamu hiyo kupitia taarifa yake, aliyoitoa leo tarehe 04 Oktoba 2024.
Amesema dirisha hilo ni kwa ajili ya kozi ambazo bado zinahitaji wanafunzi kwa mwaka huu wa masomo 2024/2025.

Amesema wamelazimika kuongeza awamu nyingine ya udahili, baada ya kupokea maombi ya kuongeza muda wa kutuma maombi ya udahili kutoka kwa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na vyuo ambavyo bado vina nafasi.

“Tume imeongeza muda wa udahili kwa kufungua Awamu ya Tatu na ya mwisho ya udahili itakayoanza tarehe 05 hadi 09 Oktoba, 2024. Tume inawaasa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi ya kudahiliwa katika Awamu ya Pili kutokana na sababu mbalimbali, watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda. Tume inaelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi,” amesema.

Prof. Kihampa amesema katika awamu hii, maombi yatatumwa kwa siku tano kuanzia kesho, vyuo vitawasilisha TCU majina ya waliodahiliwa kuanzia tarehe 13 hadi 15 Oktoba na majina ya watakaochaguliwa yatatangazwa tarehe 19, mwezi huu.

“Tarehe 19 hadi 21 Oktoba, 2024 itakuwa ni kuthibitisha udahili, kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika Awamu ya Tatu na wale walioshindwa kuthibitisha udahili wao katika awamu za udahili zilizopita,” amesema.

Katika hatua nyingine, TCU imesema majina ya wanafunzi wa shahada ya kwanza, waliodaihiliwa na vyuo vikuu katika mwaka huu wa masomo, yatatangazwa kesho, tarehe 05 Oktoba 2024.

“Waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Pili na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili katika Awamu ya Kwanza, wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia tarehe 05 hadi 21 Oktoba, 2024,” amesema Prof. Kihampa katika taarifa hiyo.

Amesema uthibitisho unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba za simu au barua pepe, zilizotumika wakati wa kuomba udahili.

About The Author

Related Posts