Viongozi wa dini kushirikiana na hifadhi ya Ruaha kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira

Viongozi wa dini kutoka Mkoa wa Iringa wamejizatiti kushirikiana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa vyanzo vya maji na ulinzi wa mazingira.

Haya yanajiri kufuatia ziara ya viongozi ndani ya hifadhi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 tangu kuzaliwa kwa hifadhi hiyo, ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini.

Wakati wa ziara, viongozi hao walishuhudia athari za shughuli za kibinadamu, uharibifu wa mazingira, na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha kupungua kwa kiwango cha maji kwenye Mto Ruaha Mkuu.

Akizungumza Kwa niaba ya Shekh wa Mkoa wa Iringa Salum Mwahuta alisisitiza umuhimu wa kulinda mto huo, ambao ni chanzo muhimu cha maji ndani ya hifadhi.

Kwa upande wake Askofu Ezekiel Mwenda, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekosti Mkoa wa Iringa, alieleza wasiwasi wake kuhusu wananchi wanaoendeleza vitendo vya kupunguza maji katika vyanzo vya mto huo, hali inayochangia kukauka kwa mto katika msimu wa kiangazi.

Afisa Mhifadhi Mkuu wa Ruaha, Rehema Kaitila, alieleza kuwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) tayari limeanza hatua za kukabiliana na tatizo la kukauka kwa Mto Ruaha.

“Kukauka kwa mto huu kumekuwa na athari kubwa, ikiwa ni pamoja na wanyama kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali ambayo inawasukuma baadhi yao kutoka nje ya hifadhi”

“Serikali pia imeanza kuchimba mabwawa ya muda ili kusaidia wanyama”Alisema

Nao baadhi ya waumini waliopata wa fursa kutembelea hifadhi hiyo wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kutunza rasilimali za maji na mazingira pamoja na kubadilishana mawazo juu ya umuhimu wa kutunza Mto Ruaha na hifadhi hiyo unakuwa salama.

Related Posts