Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alisema kwamba amesikitishwa mno na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na kundi la wanamgambo la al-Shabaab.
“Vita dhidi ya ugaidi unaofanywa na wanamgambo wa al-Shabaab bado ni swala nyeti la kiusalama linalozidi kupewa kipaumbele na serikali ya Somalia. Pamoja na kupiga hatua kubwa kupambana na magaidi hao, Somalia inakabiliwa na changamoto si haba kufuatia hatua ya kuanza kuondoka kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika (ATMIS) nchini humo.” Alisema Swan.
Maazimio ya Umoja wa Mataifa yanavitaka vikosi vya Tume ya Amani ya Umoja wa Afrika viondoke kwa awamu hadi kufikia Disemba 31 mwaka huu, na kukabidhi majukumu ya usalama kwa jeshi na polisi wa Somalia.
Soma zaidi: Maoni: Kitisho cha kuliyumbisha taifa la Kenya
Aidha kaimu mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alilaani shambulizi la kigaidi la hivi karibuni nchini Somalia ambapo maisha ya watu wapatao 37 yaliangamia.
“Kundi la al-Shabaab linazidi kuendeleza vitendo vya kikatili na mauaji dhidi ya raia wema pasipo kujali haki za binadamu, likiwepo shambulizi la hivi karibuni kabisa lililotokea tarehe 2 Agosti kwenye hoteli moja katika ufukwe wa bahari wa Lido mjini Mogadishu.”
Mgogoro wa Somalia na Ethiopia
Kuhusu mgogoro unaotokota kati ya Somalia na Ethiopia, mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa hali ya mahusiano baina ya majirani hao wawili bado inatia wasiwasi.
“Nina mashaka kutokana hali ya wasiwasi iliyopo katika eneo hilo kufuatia mkataba uliofikiwa mnamo tarehe 1 Januari baina ya Ethiopia na Somaliland. Ningependa kuzihimiza serikali ya Ethiopia na ile ya Somalia kutafuta suluhu la kudumu kwa njia ya mashauriano ya kidiplomasia kwa kuzingatia sheria ya kimataifa.” Alisema.
Soma zaidi: Al-Shabaab yadai mateka 137 wamefariki
Mgogoro kati ya Somalia na Ethiopia umesababishwa na hatua ya Ethiopia ya kukodi eneo la ufukweni la kilomita 20 katika mkoa uliojitagazia uhuru wa Somaliland.
Kwa upande wake, Somalia imesema mkataba huo unaenda kinyume na sheria na imelipiza kisasi kwa kumtimua balozi wa Ethiopia, na pia imetishia kuwatimua maalfu ya wanajeshi wa Ethiopia waliopo nchini Somalia wakisaidia juhudi za kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab.
Ethiopia inautambua uhuru wa Somaliland ambayo hapo awali ilikuwa sehemu ya Somalia.
Mwanadiplomasia huyo aliwasilisha ujumbe huo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York siku ya Alhamisi (Oktoba 3), na aliandamana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Somalia, Ahmed Moallim Fiqi, na Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia, Balozi Mohamed El-Amine Souef.