Wakenya washiriki mdahalo wa kumuondoa makamu wa rais – DW – 04.10.2024

Zoezi la kukusanya maoni ya raia lililofanyika siku ya Ijumaa (Oktoba 4) lilitazamia kuendelea siku ya pili yake, kwa mujibu wa taarifa ya karani wa bunge la taifa Samuel Njoroge.

Hii ni baada ya mahakama kuu mjini Kerugoya kuamuru kuwa Wakenya wote wanapaswa kushiriki kutoa maoni yao kwenye vituo rasmi vya kupigia kura kote nchini.

Katika Kaunti ya Nyeri anakotokea Makamu wa Rais Rigathi Gachagua, wakaazi walikusanyika barabarani walikowasha moto ili kupinga matukio ya leo.

Soma zaidi: Kenyatta: Serikali msilaumu utawala uliopita chapeni kazi

Kwa mtazamo wao hoja ya kumtimua naibu huyo wa rais ina mkono wa siasa na kamwe hawawezi kuyumbishwa kumsaliti kiongozi wao huyo.

Vurugu zilishuhudiwa pia katika Kaunti ya Nakuru pale baadhi ya raia waliposusia kushiriki zoezi hilo la kukusanya maoni.

Badala yake, vijana kadhaa walimiminika barabarani wakipiga mayowe ya kumtaka Rais William Ruto ang’atuke madarakani na sio kuondoka kwa makamu wake.

Mchakato waingia doa

Kwenye eneo la Kanda ya Ziwa, wakaazi wa Kisumu waligawanyika wakati zoezi la kukusanya maoni likiendelea kwenye chuo cha Tom Mboya.

Makamu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.
Makamu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.Picha: REUTERS

Katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, shughuli hiyo ilipita bila matukio ya vurugu.

Mjini Lodwar, idadi ndogo ya watu walijitokeza kuwasilisha maoni yao na kujaza fomu.

Kwenye kaunti jirani ya Marsabit, baadhi yao walisema wanahisi kuwa maoni yangekusanywa kielektroniki.

Soma zaidi: Gachagua awasilisha ombi kwa mahakama kusitisha mchakato wa kumuondoa

Mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Marsabit, Naomi Jillo, alisema baadhi ya viongozi wanahofia usalama wao baada ya kuorodheshwa kwenye msururu wa wabunge walioridhia hoja ya kumtimua makamu huyo wa rais.

Kwenye taarifa yake, Seneta wa Kaunti ya Nairobi, Edwin Sifuna, alikosoa vurugu hizo na kusisitiza kuwa kila mmoja ana uhuru wa kutoa maoni yake.

Bomas of Kenya ni moja ya vituo 47 ambako umma ulikuwa unawasilisha maoni yao juu ya  hoja ya kumtimua Makamu wa Rais Gachagua, lakini mitazamo ilitofautiana sana kuhusu hoja hiyo.

Mswada wa kumtimua Gachagua uliwasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse, anayemtuhumu makamu huyo wa rais kwa makosa kumi yakiwemo ya kukiuka katiba, ufisadi  na uchochezi.

Kufikia sasa saini za wabunge 291 zimekusanywa kuidhinisha kutimuliwa kwake, ingawa kisheria saini 117 pekee ndio zinazohitajika.

Mchakato wa bungeni utaendelea siku ya Jumanne wiki ijayo.

Related Posts