Tamasha la miaka 60 ya Msondo Ngoma kufanyika Oktoba 26

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Bendi maarufu ya muziki wa dansi nchini Tanzania, Msondo Ngoma Music Band, inatarajia kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake kwa tamasha maalum litakalofanyika Oktoba 26, 2024, katika viwanja vya Gwambina Lounge (zamani TCC Club) Changombe, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa bendi hiyo, Saidi Kibiriti, amesema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea kwa kasi, huku bendi ikijiandaa vilivyo kwa kuweka kambi ya mazoezi ya wiki mbili mkoani Dodoma.

“Msondo Ngoma tunajiandaa kwa sherehe kubwa ya kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa bendi yetu. Tamasha hili litakuwa na vitu vingi vipya na ubunifu ambao tumekuwa nao katika miaka 10 iliyopita, pamoja na wanamuziki wengi wapya waliojiunga na bendi katika kipindi hicho,” alisema Kibiriti.

Kibiriti alieleza pia kuwa sherehe za miaka 60 ya Msondo Ngoma zitaanza na kisomo maalum kitakachofanyika Oktoba 13, 2024, katika ofisi za bendi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuwaenzi wanamuziki waliotangulia mbele za haki. “Tutawakumbuka waimbaji wetu waliofariki kwa njia ya dua na sala maalum,” aliongeza.

Kwa upande wa maandalizi ya burudani, Kibiriti ameeleza kuwa wanamuziki wa Msondo Ngoma wanafanya mazoezi makali ili kuhakikisha kuwa tamasha hilo linakonga nyoyo za mashabiki wao kwa kupiga muziki wa ‘live’ kama ilivyo kawaida yao.

Wasanii Maarufu Kutumbuiza

Msanii maarufu Fresh Jumbe, anayeishi nchini Japan na aliyetamba na wimbo “Penzi ni Kikoozi”, atakuwa miongoni mwa waimbaji wa bendi ya Msondo Ngoma katika tamasha hilo. Jumbe amesema kuwa ataimba nyimbo nyingi alizorekodi na Msondo, na amejiandaa kikamilifu kwa tukio hilo.

Aidha, Ally Choki atatumbuiza na wimbo aliowahi kuimba na Mzee Ngurumo “Baba Ulichomtendea Mama”, pamoja na nyimbo nyingine za zamani zenye mafunzo ya wazazi. Juma Katundu, maarufu kama “JK”, pia amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia tamasha hilo kubwa.

Vikundi na Wasanii Watakaosindikiza

Tamasha la miaka 60 ya Msondo Ngoma litasindikizwa na bendi maarufu ya Twanga Pepeta, Ally Choki, Nyoshi El Sadati (Rais wa Milele), Spidoch Band ‘Wazungu Weusi’, pamoja na msanii wa Bongo Fleva Bernard Paul maarufu kama Ben Pol.

Kiingilio cha Tamasha

Kiingilio kwa tamasha hili ni Tsh 100,000 kwa VIP, Tsh 50,000 kwa viti maalum, na Tsh 15,000 kwa kawaida, huku wale watakaonunua tiketi mapema kwa mlangoni wakilipa Tsh 20,000.

Mashabiki wa muziki wa dansi na wale wanaothamini mchango wa Msondo Ngoma katika historia ya muziki wa Tanzania wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi kusherehekea tamasha hili maalum la kihistoria.

Related Posts