Kulingana na televisheni ya wanamgambo wa Houthi Al Masirah, mashambulizi hayo yamelenga maeneo 4 tu.
Marekani na Uingereza zimekuwa zikifanya mashambulizi yenye lengo la kuusitisha uwezo wa Wahouthi kuzishambulia meli, ila mashambulizi ya waasi hao kwa meli zinazopitia Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, yameendelea.
“Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) imefanya mashambulizi ikilenga ngome 15 za Wahouthi katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi nchini Yemen,” ilisema kamandi hiyo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii.
Mashambulizi tangu Novemba
Televisheni ya Al Masirah iliyosema Marekani na Uingereza zote ziliishambulia Yemen Ijumaa, awali ilikuwa imeripoti mashambulizi 4 huko Sanaa na mengine 7 Hodeida. Waandishi wa shirika la habari la Ufaransa AFP, wamesikia milipuko mikubwa katika hiyo miji yote miwili.
Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa wakizishambulia meli katika njia hiyo tangu mwezi Novemba wakidai lengo lao ni meli zilizo na mafungamano na Israel na mashambulizi hayo yanalenga kuonyesha mshikamano na Wapalestina wakati wa vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza.
Israel pia imeishambulia Yemen kutokana na hayo mashambulizi ya Wahouthi.
Mashambulizi ya Israel Hodeida mwezi uliopita yalisababisha vifo vya angalau watu 5 baada ya waasi hao kusema kwamba waliulenga kwa kombora uwanja wa ndege wa Ben Guiron nchini Israel.
Vyanzo: AFPE/AP