Kongo yaanza kutoa chanjo ya mpox baada ya mkwamo – DW – 05.10.2024

Chanjo hizo ilipangwa zianze kutolewa siku ya Jumatano kote nchini Kongo lakini mamlaka za afya ziliarifu kwamba mpango huo ulishindikana.

Mnamo Ijumaa Waziri wa Afya wa Kongo, Samuel-Roger Kamba ndiyo alitoa tarehe ya uhakika kuwa ni Jumamosi ya Oktoba 05.

Waziri wa afya wa Kongo, Samuel-Roger Kamba amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwapa chanjo watu walio katika hatari zaidi wakiwemo wahudumu wa afya.

“Tunazindua, kuanzia kesho (siku ya Jumamosi), Okotba 5 kampeni ya utoaji chanjo,” alisema Kamba alipozungumza na waandishi habari kwenye mji mkuu wa Kongo, Kinshasa.

Kampeni hiyo ya chanjo itaanzia kwenye mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini wa Goma uliopo mashariki wa Kongo, eneo ambalo ndiyo limeathiriwa zaidi na maradhi ya mpox.

Dozi zilizopokelewa zitatumika wakati nyongeza ikisubiriwa 

Taifa hilo la Afrika ya Kati limepokea dozi 265,000 za chanjo, zikijumuisha msadaa kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya.

“Itakuwa kampeni kubwa ya umma … mkakati ni kuwachanja watu walio kwenye hatari zaidi,” amesema Waziri Kamba, na kuongeza kwamba dhamira ni kuwadunga chanjo kwanza wale wenye umri mkubwa, maradhi ya kudumu na wafanyakazi wa huduma za afya.

DR Kongo Kabare | Mpox
Watoto wenye umri ya chini ya miaka mitano ndiyo wameathiriwa zaidi na mpox nchini Kongo.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Kwa idadi ya chanjo ambayo Kongo inayo hivi sasa “inatosha kuanza kuzitoa kwenye maeneo yaliyoathiriwa zaidi,” amesema Kamba.

“Bado tunasubiri chanjo zaidi,” ameongeza kusema waziri huyo.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, Kongo imerekodi kati ya visa 30,000 na 31,000 vya Mpox, pamoja na vifo vya watu 988.

Kwa mujibu wa waziri wa afya, asilimia sabini ya vifo hivyo ni vya waatoto walio na umri wa chini ya miaka mitano, na kuongeza kwamba “watoto ndiyo wameathiriwa zaidi na virusi hivyo”.

Hata hivyo chanjo zilizopo hivi sasa nchini Kongo zinazotengezwa na kampuni ya Denmark ya Bavarian Nordic ni kwa ajili ya watu wazima pekee.

Japan, Ufaransa na Marekani zasubiriwa kupeleka chanjo ilizoahidi 

Chanjo ya Mpox
Chanjo ya mpox inayotengenezwa na kampuni ya Denmark ya Bavarian Nordic.Picha: abaca/picture alliance

Kongo tayari inafanya mazungumzo na Japan, ambako chanjo ya mpox inayotumiwa kwa watu wazima na watoto imekwishaidhinishwa kutumika na kusambazwa.

“Hivi sasa tunasubiri kuwasili shehena ya pili ya chanjo ya Bavarian Nordic iliyoahidiwa na Ufaransa, ya kiasi dozi 100,000,” amesema Kamba.

“Lakini tunasubiri shehena kubwa ya zaidi ya chanjo milioni 3 iliyoahidiwa na Japan,” amesisitiza.

Rais Joe Biden wa Marekani alitangaza mwezi uliopita kwamba nchi yake inapanga kutoa msaada wa dozi milioni moja za mpox kwa mataifa ya Afrika yaliyokubwa na mlipuko wa maradhi hayo.

“Tuko tayari kutenga dola milioni 500 kuyasaidia mataifa ya Afrika kuzuia na kushughulikia mlipuko wa mpox na kuchangia dozi milioni moja za chanjo za mpox, mara moja,” aliuambia mkutano wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

WHO yaidhinisha kipimo cha mpox kusaidia mapambano ya ugonjwa huo 

Mapema siku ya Ijumaa Shirika la Afya Duniani WHO liliidhinisha kipimo cha kwanza cha ugonjwa wa mpox, hatua ambayo itayasaidia mataifa duniani yanayopambana kudhibiti maradhi hayo hatari.

DR Kongo Mpox
Janga la maradhi ya mpox.Picha: WHO/Aton Chile/IMAGO

Taarifa ya WHO imesema kipimo hicho ni muhimu katika kuongeza uwezo wa kubaini maambukizo kwenye mataifa yaliyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa mpox.

Kipimo hicho kilichotengenezwa na kampuni ya Abbot Molecular kinawezesha kubaini maambukizi ya mpox kupitia majimaji ya mwilini.

WHO imesema kukosekana vipimo kumechangia kusambaa ugonjwa huo unaosababishwa na virusi ambavyo inaaminika vinatokana na maingiliano kati ya binadamu na wanyama wa porini.

Related Posts