Kwa nini vimbunga vingi hupewa majina ya kike?

Dar es Salaam. Ni jambo linalofikirisha pale unapokuta vimbunga vingi, dhoruba au tufani mara nyingi vinapewa majina ya binadamu, na zaidi yale ya kike.

Hata kimbunga cha sasa, kinachotazamiwa kupiga katika pwani ya Bahari ya Hindi kusini mwa Tanzania kati ya Leo Mei 3 na Mei 6, 2024, kimeitwa Hidaya.

Mbali na Hidaya, vipo vimbunga vingi vilivyopopita vyenye majina kama hayo, mfano Katarina, Idai, Elida, Genevieve, Emilia, ingawa pia vipo kadhaa vyenye majina ya kiume au yasiyo na jinsi kama Jobo, Erick, Kenneth na mengineyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa la Duniani (World Meteorological Organisation), kuna orodha ya majina inayozunguka kulingana na matukio kama hayo yanapotokea.

Mtindo huu wa kuita majina vimbunga vya kitropiki ulianza miaka mingi iliyopita. Ilikuwa ni kwa lengo la kubainisha taarifa za athari za vimbunga. Majina yanatajwa kuwa njia rahisi ya kukumbuka kuliko namba na mambo ya kiufundi.

Hata hivyo, si kila kimbunga kinakuwa kikubwa kiasi cha kupewa jina, ila vile tu vinavyotarajiwa kusababisha hasara kubwa na inaelezwa kuwa mara nyingi vyenye majina ya kike huwa ni hatari zaidi.

Kwa miaka mingi, vimbunga vilikuwa vikipewa majina bila kujali jinsi, kuna wakati wataalamu wa hali ya hewa walikuwa wakiviita vimbunga hivyo majina ya watakatifu, wake zao, wapenzi au watu wengine mashughuli.

Maandiko mbalimbali yanaeleza kuwa vimbunga vingi hupewa majina ya jinsi ya kike kutokana na imani iliyokuwepo miaka mingi kuwa wanawake hawatabiriki.

Miongo zaidi ya 70 iliyopita kulikuwa na wataalamu wachache wa hali ya hewa wanawake, kada hiyo ilitawaliwa na wanaume ambao ndio walikubaliana vimbunga vipewe majina ya kike, wakiamini ni vigumu kutabiri kwa ufasaha ni uelekeo gani kitaelekea, kama walivyoamini kwa mwanamke.

Hata hivyo dhana juu ya mwanamke kutotabirika haikuwafurahisha wanaharakati wa haki za kijinsia ingawa haikukoma, isipokuwa kwa maeneo ya Bahari ya Pasifiki, iliboreshwa na kuongezewa tafsiri inayoakisi sifa za wanawake walio wengi.

Wengine wanafananisha dhoruba kama mchezo au uchokozi wa kimahaba ambao mwanamke anaweza kumfanyia mpenzi wake wa kiume na katika muktadha huo mwenza ni kingo ya bahari.

Kuna wakati Marekani kuliibuka mjadala kuwa kimbunga au janga la asili likipewa jina la kiume kunaweza kuwa na madhara zaidi kwa wanaume wanaoitwa jina hilo, kuwa wanaweza kuogopwa sawa na ukubwa wa athari za janga lililotokea.

Related Posts