Waziri Bashe amesema hayo jana baada ya kuzindua Kituo hicho kinacholenga kutoa mafunzo ya ubunifu na uzalishaji wa bidhaa za mkono zitokanazo na singa za Mkonge, uzalishaji nzi chuma, utengenezaji wa karatasi, mafunzo ya ukataji na uchakataji Mkonge.
Amesema kituo hicho kinahitaji kuwa na vifaa ili kina mama, wenye ulemavu na vijana wanaozalisha bidhaa mbalimbali wakija wakute vifaa vyote muhimu ambapo pia watatumia kituo hicho kama sehemu ya kuzalishia mali kisha kwenda kufanya biashara zao nje.
“Naagiza tupate vifaa vyote muhimu ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kufanya shughuli ndogo ndogo za uzalishaji mkonge ili vikundi vya wajasiriamali kina mama na vijana wakipata mkopo wa asilimia 10 wa halmashauri, wana uwezo wa kwenda kununua singa za Mkonge au malighafi hawahitaji kununua mashine, watazikuta hapa.
“Mkonge ni zao muhimu sana katika uchumi wa nchi, zipo bidhaa nyingi zinazotokana na
mkonge. Bodi imeingia makubaliano na wenzetu ambao wamekuwa wakifundisha namna ya kutumia mabaki ya Mkonge katika kuzalisha karatasi,” amesema Mh. Bashe.
Mh. Bashe amesema Serikali imeweka dhamira kupitia maombi ya bodi takribani Sh milioni 600 kwa ajili ya kuweka Kituo Atamizi Tanga na Zanzibar ambapo Tanga itakuwa
kituo ambacho vitawekwa vifaa vyote vidogo vidogo vya kuongeza thamani Mkonge na
mazao mengine madogo madogo ya kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mkonge wa TSB, Olivo Mtung’e amesema Kituo hicho kimeanzishwa Tanga kwa sababu Mkonge unalimwa zaidi na ndiyo Makao
Makuu ya TSB.
Amesema Kituo hicho Atamizi lengo lake kwanza ni kuwawezesha vijana, wanawake na
wenye ulemavu kwa ajili ya kujiajiri lakini pia watakwenda kuwasaidia ambao wanazalisha
Mkonge hasa kwa upande wa Tanga ambao walikuwa wanakosa soko la kuuza Mkonge nje.
“Soko letu bado linategemea zaidi kuuza nje huku ndani matumizi siyo makubwa sana
lakini tunatambua kuwa vijana wetu, kina mama hawana ajira za kuwaingizia kipato kwa hiyo tunategemea kituo hiki kuwa na watu ambao watajiajiri. Pia tutaongeza matumizi ya zao la Mkonge kwa upande wa ndani.
“Lakini pia kituo hiki ni sehemu ya kwanza tu kuna vituo vingi vinakuja kutakuwa na mashine ya kutengeneza bidhaa za mkono za kufuma kama vile Kamba na cha pili kinaratajiwa kuanzishwa hapa hapa Tanga kwa ajili ya kutengeneza karatasi na gypsum na vitu vya kuezekea,” amesema Olivo.