Kibu nje Simba ikiivaa Mtibwa Sugar

YUKO wapi Kibu Denis? Hilo ndilo swali ambalo mashabiki wa Simba wanajiuliza baada ya kuuwekwa wazi kikosi chao ambacho kitacheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar muda huu.

Uvumi wa Kibu kuhusishwa na Yanga ndio sababu iliyowafanya mashabiki hao kuhoji kuhusu mshambuliaji huyo hapa Chamazi, kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mashabiki hao wameanza kuhoji tangu saa 9:00 alasiri (saa moja kabla ya mchezo) wakati ambao kikosi chao kitakachoivaa Mtibwa Sugar kikiwekwa wazi katika mitandao ya kijamii.

Justine Mush, mmoja wa mashabiki hao kutokuwepo kwa Kibu kumemfanya kuwa na hofu, huku akiwa na imani kwamba  ‘Mkandaji’ huyo bado anahitajika kwenye kikosi chao.

“Wasijekuwa wenzetu (Yanga) wametuzidi kete, ni kweli hali yetu ni mbaya lakini viongozi wetu wanatakiwa kuwa macho na wachezaji wetu muhimu,” amesema shabiki huyo.

Kwa mujibu wa taarifa, inaelezwa Kibu ambaye mkataba wake upo ukingoni Simba yupo katika mazungumzo ya hatua za mwisho kutua Jangwani.

Licha ya kuwepo kwa hilo, vigogo wa Simba wanatajwa kujaribu bahati yao kumbadili mawazo mshambuliaji huyo ambaye alikuwa kipenzi cha Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Kikosi cha kwanza cha Simba kilichoanza ni Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Che Malone, Hussein Kazi, Mzamiru Yassin, Willy Onana, Fabrice Ngoma, Freddy Michael, Said Ntibazonkiza na Edwin Balua.

Akiba ni Abel, Duchu, Kennedy, Henock, Hamis, Kanoute, Karabaka, Chasambi na Jobe.

Related Posts