Atolewa uvimbe wa kilo tano tumboni alioishi nao miaka 10

Geita. “Nimezaa watoto 11 lakini mtoto wangu wa mwisho niliyemzaa mwaka 2010 nilikuwa nipoteze maisha, maana nilitokwa na damu nyingi sana, nikazimia mara tatu na wakati wote wa mimba damu ilikuwa inavuja, sikujua tatizo.”

Haya ni maneno ya Eveline Paulo, mkazi wa Biharamulo mkoani Kagera aliyetolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tano tumboni.

Uvimbe huo alioishi nao kwa miaka 10 bila matibabu, ulikuwa umekaa nje ya kizazi.

Akizungumza na Mwananchi, akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita baada ya kufanyiwa upasuaji, Eveline amesema tumbo lake lilikuwa limejaa na alihangaika kwenda hospitali mbalimbali lakini hakupata huduma kutokana na kusumbuliwa na shinikizo la damu.

“Nimehangaika kwenda hospitali huko Biharamulo na Mwanza, lakini kila wakitaka kunihudumia presha inapanda, narudishwa nyumbani, mwisho nikaamua kuishi na hali hiyo hadi nikaona kawaida, lakini nilikuwa nateseka sana,” amesema mama huyo.

Hata hivyo, amesema hivi karibuni alienda kumtembelea mwanawe aishie Geita na akamsimulia tatizo lake na mwanawe akaamua kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi na baada ya vipimo kuonyesha uvimbe alikokuwa nao tumboni ni mkubwa, madaktari wakaelekeza afanyiwe upasuaji kuuondoa.

Akizungumzia upasuaji huo uliochukua saa mbili na nusu, Dk Isaack Ajee, bingwa wa magonjwa ya wanawake ameasema uvimbe aliokuwa nao Paulo ulikuwa wa sentimita 38 na kama ingekuwa ni mimba, ni sawa na ya miezi tisa.

“Lakini hata hivyo, uzito wa uvimbe huu unazidi ule wa mtoto anayezaliwa, tunashukuru Mungu tumemaliza salama na  afya ya mama kwa sasa iko sawa na akiendelea hivi baada ya siku mbili ataruhusiwa kutoka hapa hospitali,” amesema daktari huyo.

Dk Ajee amesema uvimbe huo ulikuwa na uzito wa kilo tano na ulikuwa pembeni ya kizazi hali iliyosababisha kukibanwa.

Amesema mama huyo pia alikuwa na uvimbe mwingine mdogo ndani ya kizazi.

“Tulibaini ana fibroids na ilikuwa kubwa, ilikuwa pembeni ya kizazi lakini pia ndani ya kizazi kulikua na vimbe ndogondogo hii ya pembeni ya kizazi ilikuwa ikipokea damu kutoka sehemu nyingine za mwili.”

“Upasuaji huu tuliufanya na wataalamu wenzangu watatu, mwanzoni tulihoifia unaweza kujishikiza kwenye matumbo au kwenye kibofu cha mkojo au unaweza kushika sehemu nyingine tofauti, ndiyo maana tuliingia watatu ili isijetokea tatizo.

“Tulihakikisha tunautoa vizuri na tumeikuta imejishikisha kwenye kizazi japo ni nje, lakini kizazi kilikuwa kimebanwa na ndani ya kizazi kulikua na vimbe ndogondogo,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Dk Ajee, kutokana na uvimbe kuwa nje ya kizazi, kulimfanya mwanamke huyo asipate tatizo kama lile la uvimbe unaoota ndani ya kizazi.

Amesema endapo uvimbe huo usingetolewa na ukaendelea kuvimba, ungemfanya apate ugonjwa ya wa UTI mara kwa mara kutokana na kukandamiza kibofu, kupata choo kigumu na wakati mwingine kufunga.

Pia angeweza kupata msukumo kwenye kizazi na kushindwa kulala vizuri, ameongeza daktari huyo.

Amesema mwanamke anayeugua ugonjwa wa aina hiyo asipopata huduma sahihi, husababisha tumbo kujaa gesi na kushindwa kuhema vizuri na mara chache uvimbe wa aina hiyo husababisha pia saratani.

Sababu mwanamke kupata ‘fibroids’

Dk Ajee amesema hakuna sababu maalumu za kitaalamu zinazoonyesha husababishwa na nini, hata hivyo, anasema inaweza kumpata mtu kutokana na historia ya familia yake, pia wanawake wenye vitambi, wenye uzito mkubwa na wasiozaa (wagumba) au wanaotumia dawa za vichocheo wako hatarini zaidi.

Kuna dawa zaidi ya upasuaji?

Kwa mujibu wa Dk Ajee, tiba sahihi ya kutibu ‘fibroads’ au ‘mayoma’ ni mgonjwa kufanyiwa upasuaji na hakuna dawa ya kunywa ya kukwepa upasuaji.

“Kilichopo ni kwamba wapo watu wana mayoma na wakati mwingine inakuwa kubwa na anatokwa na damu, akiwa kwenye shatua hii anapewa dawa ya kuchoma ili uvimbe usinyae na baada ya hapo anafanyiwa upasuaji kuitoa. Dawa hii haiondoi uvimbe kazi yake ni kuufanya usinyae tu,” amesema Dk Ajee.

Hivyo, ameonya watu wasidanganywe kwamba kuna dawa za kunywa kuuondoa zaidi ya kufanyiwa upasuaji.

“Na kuna watu wanaosema wanatibu uvimbe kwa kuwapa wagonjwa dawa za kunywa, hilo ni kosa kimatibabu kwa kuwa mpaka sasa hakuna dawa ya kutibu ‘fibroid zaidi ya kufanya upasuaji na kuzitoa,” amesema.

Tofauti uvimbe ndani ya kizazi na nje ya kizazi

Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa, uvimbe ukitokea ndani ya kizazi, mgonjwa atakuwa akitokwa na damu nyingi wakati wa hedhi na kupata maumivu makali huku ule wa nje ya kizazi, mgonjwa hapati maumivu ila athari yake zinaweza kuwa kubwa endapo utajishikiza kwenye kizazi na husababisha maumivu kwa sababu damu haisambai.

Akizungumzia siku tatu walizofanya huduma za mkoba katika Hospitali ya Mkoa wa Geita, Dk Ajee amesema wamewahudumia wanawake zaidi ya 150 na wengi wao wakiwa na changamoto za uzazi na hedhi, kutokwa uchafu sehemu za siri na uvimbe kwenye kizazi.

Dk Ajee amewataka wanawake wanaobainika kuwa na matatizo hayo wasikate tamaa ya kutafuta huduma za tiba.

Related Posts