Rais wa Zanzibar aipongeza Benki ya Absa Tanzania kuboresha afya ya mama na mtoto.

 

Na mwandishi wetu.Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Benki ya Absa Tanzania kwa mchango wake wa shs milioni 150 kuchangia kampeni ya ‘Uzazi ni Salama’ yenye lengo la kuboresha afya ya mama na mtoto wakati wa ujauzito na kujifungua.

Mheshimiwa Rais Mwinyi alitoa pongezi hizo katika hafla ya tatu ya shukurani na uchangishaji fedha wa kampeni hiyo, iliyoandaliwa na Shirika la Amref Tanzania, Wizara ya Afya Zanzibar, kwa udhamini mkuu wa Benki ya Absa Tanzania na kufanyika katika Ikulu ya Zanzibar, jana.

“Leo tumekusanyika hapa kwa lengo la kuunga mkono juhudi za kuokoa maisha kupitia kampeni hii, iliyoanzishwa mwaka 2020 ikiwa na lengo la kukusanya fedha kiasi cha shs Bilioni 1.

“Aidha nimefahamishwa, mwezi juni mwaka huu, Amref, wizara yetu ya afya pamoja na Benki ya Absa Tanzania wakiungwa mkono na wadau kadhaa walitoa vifaa tiba vyenye thamani ya shs milioni 262.6 kwa ajili ya vituo vya afya 28 katika mikoa mitano ya Zanzibar, niwashukuru Amref Tanzania, wadhamini wakuu Benki ya Absa Tanzania na wadau wote kwa kujitolea kuunga mkono jitihada ya serikali ya Zanzibar katika kuboresha huduma za afya”, alisema Rais Mwinyi.

Pamoja na hayo alisema ni jambo la kutia moyo kuona Zanzibar ikiwa kwenye njia sahihi ya kufikia malengo endelevu (SDG) 2030 ya kupunguza vifo vya wajawazito hadi chini ya vifo 70 kwa vizazi hai 100, vifo vya watoto wachanga hadi kufikia 12 kwa kila vizazi 1000 na vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi 25 kwa kila vizazi hai 1000 kufikia 2030.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bwana Obedi Laiser alisema wametoa msaada kuunga mkono juhudi zinazofanywa za serikali za mbili za, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwekeza katika sekta ya afya hususan katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

“Benki ya Absa Tanzania tunaenda sawa na lengo la taasisi yetu lisemalo ‘Kuiwezesha Afrika na Tanzania ya kesho kwa pamoja, hatua moja baada ya nyingine’ hapa tukihakikisha jamii yetu inapata huduma za afya stahiki.

“Lakini pia msaada huu unaenda sambamba na ahadi yetu ya chapa tuliyoizindua hivi karibuni isemayo ‘Stori yako ina thamani’, hivyo kwa kuunga mkono juhudi hizi, tunaamini tunazisaidia serikali zetu katika kuandika stori zake zile zinazohakikisha watanzania wote wanapata huduma bora za afya”, alisema Bw. Laiser.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dk. Florence Temu alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kukubali, kujitoa na kuunga mkono kampeni ya Uzazi ni Maisha tokea ilipoanzishwa mwaka 2020.

“Niwashukuru pia wadhamini wakuu, Benki ya Absa pamoja na wafadhili wetu wengine waliokuwa nasi tokea mwanzo kufanikisha malengo ya kampeni hii yenye kauli mbiu ya ‘Changia Vifaa Tiba kwa Uzazi Salama’ ambapo kati ya malengo yetu ya kukusanya kiasi cha shs Bilioni 1, hadi sasa tumeshapokea ahadi zenye thamani ya shs 989,831,145, Zaidi ya asilimia 98.9 ya malengo yetu tukipokea kiasi cha shs 740,457,422 sawa na asilimia 75”, alisema Dk. Florence.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassoro Mazrui, Naibu Waziri, Mhe. Hassan Khamis Hafidh, Katibu Mkuu, Dk. Mngereza Mzee Miraji, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na kitaifa ya maendeleo, watendaji na watumishi wa serikali na mashirika ya umma.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi (wa pili kulia), akikabidhi cheti cha shukurani kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser kwa kutambua mchango wa benki hiyo katika kuwezesha kampeni ya ‘Uzazi ni Maisha’ iliyoanzishwa na Shirika la Amref Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Zanzibar. Ilikuwa ni katika hafla ya shukurani na uchangishaji fedha iliyofanyika katika Ikulu ya Zanzibar, jana. Wengine kutoka kushoto ni, Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Mazrui, Mwenyekiti wa Bodi ya Amref, Bw. Anthony Chamungwana na Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dk. Florence Temu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati) na wengine kutoka kushoto; Mwenyekiti wa Bodi ya Amref Tanzania, Bw. Anthony Temu, Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Mazrui, Mkurugenzi Mkazi wa Amref Tanzania, Dk. Florence Temu na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser, wakifanya dua katika hafla ya shukurani na uchangishaji fedha wa kampeni ya ‘Uzazi ni Maisha’ iliyofanyika katika Ikulu ya Zanzibar, jana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, akihutubia katika hafla ya shukurani na uchangishaji fedha ya kampeni ya Uzazi ni Maisha iliyofanyika katika Ikulu ya Zanzibar, jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser, akizungumza kuhusu udhamini na malengo ya benki hiyo katika kuiwezesha kampeni ya ‘Uzazi ni Maisha’ iliyoanzishwa ma Shirika la Amref Tanzania pamoja na Wizara ya Afya Zanzibar, katika hafla ya shukurani na uchangishaji fedha kwa ajili ya kampeni hiyo katika Ikulu ya Zanzibar, jana. Kampeni hiyo ina lengo la kuboresha afya ya mama na mtoto wakati wa ujauzito na kujifungua

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati),akipozi kwa picha ya kumbukubu na baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Absa Tanzania, pamoja na viongozi wengine, mara ya baada ya hafla ya shukurani na uchangishaji fedha ya kampeni ya ‘Uzazi ni Salama’ iiyofanyika Ikulu ya Zanzibar, jana.

Related Posts