UDINI NI HATARI, KUCHOMA NGUO NI UTOTO

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewahimiza Watanzania kuendelea kushirikiana na CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kimeonyesha kwa vitendo uwezo wa kuongoza nchi na dhamira ya kuwahudumia wananchi wanyonge.

Dkt. Nchimbi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Lamadi, Wilaya ya Busega na Kata ya Dutwa, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, kwa nyakati tofauti leo, tarehe 6 Oktoba 2024.

Hii ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu katika mkoa huo, ambapo alieleza kuwa CCM imekuwa ikiandaa viongozi wake kwa ufanisi.

“Kiongozi aliyeandaliwa vizuri hueleza mipango yake waziwazi anapopewa nafasi: ‘Nikitwaa madaraka, nitafanya moja, mbili, tatu.’ Lakini kiongozi ambaye hajakomaa, anapewa nafasi ya kuzungumza na kuanza kuhamasisha maandamano, kuchoma nguo, au kuzomea watu, hapo unajua bado hajakomaa na anahitaji muda wa kujifunza zaidi.”

“Katika CCM, hatuna viongozi wanaoshikilia madaraka kwa miaka 40. Viongozi wanachaguliwa, wanapungua, na wengine wanapewa nafasi. Ukiangalia baraza la kwanza la mawaziri la Tanganyika, leo hii hakuna hata mmoja aliyebakia kwenye baraza. Kila uongozi unaleta sura mpya. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu wa miaka mitano iliyopita, leo hayupo. Hii ndiyo CCM.”

Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa hii ndiyo sababu CCM kinaendelea kuwa chama chenye nguvu, kijana kuliko vyama vingine nchini, kwani uhai wa chama unategemea wanachama na viongozi wake.

“Huwezi kusikia mwanachama mkongwe wa CCM akishabikia udini au ukabila. Lakini kuna viongozi wa vyama vingine ambao wameonyesha kushabikia hayo kwa sababu hawana historia ya kuijenga nchi hii, wala hawajui maumivu ya watu wake. Wao hawaitazami nchi kwa mbali, ndiyo maana wanaweza kutoa matamshi bila kujali madhara yanayoweza kutokea,” aliongeza Balozi Nchimbi.         

Related Posts