Kipa wa Yanga Djigui Diarra amepata mshindani wa maana kwenye vita ya ‘cleansheet’ kwenye ligi ambaye ni kipa wa Coastal Union, Ley Matampi, ambaye ni gumzo kwa sasa kutokana na kazi bora.
Sasa kocha aliyemleta nchini Mwinyi Zahera amesimulia sakata la usajili wake. Kocha huyo ambaye kabla ya kutua Namungo alitokea Coastal Union anasema;
“Tulipokuwa kwenye maandalizi ya mwanzo ya msimu kwenye zile mechi za kirafiki Coastal ndio tulianza kuona tatizo la makipa wetu, hasa pale tulipoanza kuruhusu mabao ambayo tathimini yetu iliona ni makosa ya makipa,”anaeleza Zahera.
“Tukiwa kwenye kusaka kipa mpya akaletwa kipa mmoja kutoka Ghana tukamtaka tumfanyie majaribio mazoezini baadaye tukaona bado sio mtu muafaka kukaa langoni kwetu, tukamuacha kiwango chake kilikuwa cha kawaida sana,” anaeleza Zahera.
“Uongozi ukaniuliza kama kuna kipa namjua niwatafutie, nikawaambia kuna kipa mmoja mkubwa sana kule Congo Leyi Matampi alikuwa anaichezea FC Lupopo ambao ni wapinzani wakubwa na TP Mazembe, lakini baadaye wakatofautiana na akaamua kuondoka Lubumbashi na kurudi Kinshasa.
“Nikawaambia wamuangalie video zake na wakiona anafaa nijaribu kuongea naye nimlete Coastal Union, kweli wakaangalia haraka wakarudi kwangu wakaniambia kocha huyu kipa ni hatari sana tunaweza kumpata kweli? Walisema hivyo wakihofia juu ya fedha za kumlipa.”
“Niliwasiliana naye na nikamueleza kwamba hii itakuwa nafasi nzuri kwake kujitangaza ligi ya hapa kama kupata fedha nyingi labda icheze timu kama Simba,Yanga au Azam lakini hizi zingine malipo yake ni ya chini sana.
“Akaniambia basi niongee na Coastal wamlipe dola 4000 kwa mwezi (sh 10.3 milioni) nikacheka nikamwambia hilo halitawezekana kabisa nikamwambia faida ambayo ataipata kubwa, atajitangaza kwa kuwa ligi ya hapa mechi zote 30 zinaonyeshwa moja kwa moja hii itampa fursa kubwa ya kujiuza kwa klabu zingine.
“Kwa heshima yangu na mimi nilikuwa pale Matampi akakubali kwa kaisi kidogo sana, viongozi wa Coastal Union walifurahi sana wakamtumia tiketi akaja nchini kuja kuanza kazi.”
Baada ya Matampi kutua nchini na kuanza kazi utata ukaja katika ukamilifu wa kupata vibali vyake jambo ambalo lilitumia muda mrefu, kumbe ndani yake kukawa na figisu kutoka kwa kigogo mmoja kumlinda kipa ambaye alikuwa anacheza klabuni hapo.
“Ile mechi ya kwanza ya Coastal Union na Simba pale Dar es Salaam nakumbuka mpaka leseni ya ligi ilikuwa tayari na kipa ameshaandaliwa tangu tukiwa mazoezini lakini ikaja taarifa kutoka kwa kiongozi mmoja akasema Matampi asicheze tena hebu fikiria kuanzia kule kama angekuwa anacheza ingekuwaje?
“Baadaye ikaja kujulikana kwamba Matampi ni kama alikuwa anakwamishwa kwa makusudi kulinda nafasi ya kipa mmoja ambaye Matampi alipoanza kudaka tu hakuna aliyetaka tena kumuona yule kipa anadaka mpaka akaamua kuondoka na huko aliko pia hafanyi vizuri sana ana makosa yale yale.”
“Mimi naona watu wanamshangaa Matampi lakini mimi sioni kama anafanya maajabu labda kwa kuwa watu hawakuzoea kuona kipa bora kama huyo anaichezea klabu kama Coastal Union, huyu ni kipa ambaye pale Simba Yanga au hata Azam anacheza vizuri sana kwa ubora wake amecheza mechi nyingi kubwa za ushindani.
“Kule Congo ukiondoa Kidiaba (Robert) ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa, yeye ndie kipa ambaye anafuata kwa jina kubwa na uwezo wake kile anachofanya Coastal Union ni sehemu tu ya kazi yake kama angeanza kwa wakati pale Coastal Union sidhani kama wangeniondoa, niliondolewa kutokana na timu kuruhusu sana mabao.
Zahera anafichua kuwa wakati akiwa kocha wa Yanga aliwahi kumpendekeza Matampi asajiliwe lakini kutokana na hali ya kiuchumi wa wakati huo dili hilo likashindikana.
“Wakati nikiwa Yanga tulipokuwa tunapiga hesabu za kusajili kipa mzuri wa maana jina la kwanza lilikuwa ni Matampi, lakini kutokana na hali ya fedha wakati huo viongozi wakashindwa kumalizana naye.”
Hivyo wakamuomba asubiri kwanza wakusanye fedha lakini baada ya muda akapata ofa kubwa ya kwenda Saudi Arabia kwa klabu ya Al-Ansar iliyomuwekea fedha nyingi baada ya kumkosa ndio tukaenda kumchukua yule kipa wa Kenya Farouk Shikhalo.