MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameipongeza Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa zinazofanyika kwenye kuwekeza katika sekta ya elimu nchini.
Prof Ndakidemi ameyasema hayo alipokuwa Mgeni rasmi kwenye Mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Masoka iliyopo Halmashauri ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Aliipongeze Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na sekta ya elimu kwa jamii hapa nchini na kudai kuwa kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu, serikali imejitoa kimasomaso kubeba gharama za kuwekeza kwenye miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara, mabweni, nyumba za waalimu, kutoa vifaa vya kufundishia na kuongeza ajira kwa walimu.
Vilevile, serikali imeendelea kutoa elimu bila ada kwa watoto wote kuanzia shule za msingi hadi kidato cha sita na kudai kuwa hatua hizo za serikali zimeongeza chachu ya kukuza na kuhamasisha jamii kuipenda elimu.
Mbunge aliipongeza serikali kwa uwekezaji mkubwa katika Shule ya Sekondari Masoka ambapo hivi karibuni wameipandisha hadhi na kuwa Masoka High School ambapo kwenye kufanikisha hilo Serikali imetoa shilingi milioni 393,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, mabweni mawili na matundu 16 ya vyoo.
Katika hafla hiyo, Profesa Patrick Ndakidemi aliwapongeza sana Walimu wa Shule ya Sekondari Masoka (wakiongozwa na bodi ya shule na Mwalimu Mkuu Ahmed Litinji) kwa uchapakazi hodari kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa elimu bora kwa wanafunzi, jambo ambalo limeifanya Sekondari ya Masoka kuwa shule inayoheshimika kitaaluma katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro na hapa nchini.
Katika kukabiliana na changamoto ya michezo hapo shuleni, Mbunge alitoa fedha taslimu kutengeneza magoli katika viwanja vya michezo, mipira na seti ya jezi.