Umetimia mwaka mmoja tangu mashambulizi ya Oktoba 7 – DW – 07.10.2024

Maandamano ya kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja wa mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel na vita katika Ukanda wa Gaza yamefanyika katika miji ya Berlin, Düsseldorf, Hamburg na Munich na mengine yakigubikwa na ghasia.

Polisi walishika doria ili kuhakikisha maandamano hayo yanafanyika kwa amani, japo yaligeuka na kuwa ya vurugu mjini Berlin wakati waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina walipowarushia polisi mawe na chupa. Polisi ya Ujerumani imesema takriban watu 3,500 walishiriki maandamano hayo mjini Berlin. 

Soma pia: Israel yashambulia vikali Hezbollah mjini Beirut

Katika eneo la Kreuzberg, polisi iliwatahadharisha watu waliokuwa wakishiriki maandamano hayo kuwa, “usalama wa umma uko hatarini,” na kuongeza kuwa baadhi ya waandamanaji walifanya vitendo vya uvunjivu wa sheria.

Takriban watu 3,500 walishiriki katika maandamano yalioandaliwa chini ya kauli mbiu “maandamano dhidi ya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza,” idadi hiyo ikiwa zaidi ya watu 1,000 ambao awali walijiandikisha kushiriki.

Polisi yakabiliana na waandamanaji waliozua vurugu

Berlin | Maandamano | Palestine
Maafisa wa polisi mjini Berlin wakikabiliana na waandamanaji wakati wa maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina Picha: Christian Mang/REUTERS

Maandamano hayo yalitarajiwa kuvutia watu wapatao 1,000 na yalianza katika wilaya ya Kreuzberg kabla ya kuelekea eneo la Neukölln, lenye idadi kubwa ya watu wa jamii ya Kiarabu.

Maandamano tofauti ya kuiunga mkono Israel yaliyopewa jina “pamoja dhidi ya uhalifu wa Hamas kwa raia wa Israel na Wapalestina na kwa ukombozi wa mateka na kumaliza utawala wa Hamas katika ukanda wa Gaza,” yalitarajiwa kuhudhuriwa na watu 500 katika eneo la kati, mjini Berlin.

Soma pia: Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel

Mzozo huo ulioanza wakati wapiganaji wa kundi la Hamas walipoivamia ardhi ya Israel mnamo Oktoba 7, mwaka 2023 na kuwaua takriban watu 1,200 na kuwachukua mateka 250 unatimiza mwaka mmoja leo Jumatatu.

Israel ilijibu kwa kufanya mashambulizi makubwa katika ukanda wa Gaza ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 41,800 kulingana na Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas.

Wizara hiyo ya afya haitofautishi kati ya vifo vya wapiganaji wa Hamas na raia wa kawaida na takwimu hizo haziwezi kuthibitishwa kwa njia huru.

Related Posts